Zelenskiy: Mwaka 2025 kuamua atakayeshinda vita Ukraine
19 Novemba 2024Zelenskiy ameyasema haya alipokuwa akilihutubia bunge la Ukraine wakati ambapo vita hivyo vimeingia siku yake ya elfu moja.
Akiwasilisha kile kilichoitwa "mpango wa uthabiti" kwa Ukraine, Zelenskiy amesema kwamba Waukraine hawastahili kamwe kumkubalia yeyote yule atilie shaka uthabiti wa taifa lao.
Rais huyo wa Ukraine amesema kwa sasa inaamuliwa ni nani atakayeshinda na hilo litaonekana mwakani.
Zelenskiy ameyasema haya wakati ambapo Urusi imezidisha mashambulizi ya angani katika miji ya Ukraine kuelekea kipindi cha msimu wa baridi na zaidi ya hayo, imepokea zaidi ya wanajeshi 10,000 kutoka Korea Kaskazini kuisaidia katika mapambano.
Uhuru wa Ukraine hautouzwa
Huku kukiwa na atiati kuhusiana na misaada ya kijeshikwa Ukraine kutoka Marekani, Zelenskiy amesema Kyiv haistahili kumpa mtu yeyote yule nafasi ya kuamua mustakabali wa nchi hiyo. Matamshi ya rais mteule wa Marekani Donald Trump kwamba analenga makubaliano ya haraka ili avimalize vita hivyo, yameibua wasiwasi kwamba Marekani inaweza kuilazimisha Ukraine ikubali kuachia baadhi ya maeneo yake.
"Hatubadilishani uhuru wa Ukraine, usalama au mustakabali na chochote kile. Hatutoiacha haki ya Ukraine kwa eneo lake zima na bila shaka hatutomkubalia yeyote yule aitumie nchi yetu katika mapambano ya kabla uchaguzi Ulaya. Hakuna atakayeshinda kwa gharama ya Ukraine ila upo uwezekano wa kushinda pamoja na Ukraine, hiyo ndiyo njia ya pekee," alisema Zelenskiy.
Zelenskiy lakini amesema kwamba huenda nchi yake ikasubiri hadi mwisho wa utawala wa Rais Vladimir Putin ili iweze kuyarudisha katika himaya yake maeneo yaliyochukuliwa yanayotambulika kimataifa.
Haya yanafanyika wakati ambapo Urusi Jumanne imesema Ukraine imerusha makombora sita ya masafa marefu yaliyoundwa Marekani aina ya ATACMS, katika eneo la magharibi mwa Urusi la Bryansk.
Ukraine haijathibitisha kutumia makombora hayo ambayo huenda yakawa ya kwanza tangu Rais Joe Biden kutoa idhini ya Kyiv kuyatumia kushambulia ndani ya Urusi.
Vifo eneo la kaskazini mashariki la Sumy
Urusi kupitia taarifa ya wizara yake ya mambo ya nje imesema, hatua ya Marekani kuidhinisha kutumika kwa makombora hayo ni ya kizembe na itaipelekea Urusi kujibu.
Matamshi haya ya Urusi yanakuja wakati ambapo watu 12 wamefariki dunia kutokana na shambulizi la Urusi la ndege isiyokuwa na rubani usiku wa kuamkia Jumanne katika eneo la kaskazini magharibi mwa Ukraine la Sumy.
Kulingana na polisi ya Ukraine, shambulizi hilo katika mji mdogo unaopakana na Urusi wa Hlukhiv limesababisha watu 13 kujeruhiwa wakiwemo watoto watatu.
Vyanzo: Reuters/AFP