Zelensky akasirishwa na NATO kusuasua kuikubali Ukraine
11 Julai 2023Zelensky, ambaye atajiunga na mkutano huo wa siku mbili unaofanyika Vilnius, ameshutumu kile alichokiita "hatua isiyokuwa na mantiki" ya kusitasita kwa baadhi ya viongozi wa NATO kutoa mwelekeo wa muda wa Ukraine kujiunga na jumuiya hiyo.
Kupitia ukurusa wake wa mtandao wa Twitter, Zelensky ameandika kuwa "kutokuwa na uhakika ni udhaifu," na kwamba ataliweka suala hilo mezani kwenye mkutano huo.
Soma zaidi: NATO: Kuungwa mkono Ukraine ni jukumu muhimu
Biden kukutana na Zelensky
Jumuiya hiyo imeonesha mshikamano na kuiunga mkono Ukraine katika vita vyake dhidi ya Urusi, japo baadhi ya wanachama wake - hasa Rais wa Marekani Joe Biden - wameonekana kupinga wazo la kuipa muda maalum Ukraine wa kujiunga na NATO.
Badala yake, mkutano huo wa kilele wa Vilnius unatarajiwa kuendelea kutoa ahadi ya silaha zaidi kwa Ukraine na kuipa thibitisho nchi hiyo kwamba hatimaye itakuwa moja ya wanachama wake mara tu watakaposhinda vita dhidi ya Urusi.