AfD wameondoka na ushindi wa ajabu
14 Machi 2016Matokeo ya uchaguzi wa majimbo matatu,Baden-Wuerttemberg,Rhineland Palatinate na Saxony Anhalt si ya kustaajabisha.Yanatoa picha ya zahma iliyozuka katika jamii kufuatia sera za kansela Angela Merkel za kuacha wazi mipaka . La maana hapo ni kwamba wananchi wengi zaidi wameteremka vituoni safari hii ikilinganisahwa na miaka mitano iliyopita. Si kwa faida ya vyama vikuu lakini; wapiga kura wengi wamevipa kisogo vyama hivyo na kukipa kura zao chama cha siasa kali za mrengo wa kulia "Chaguo Mbadala kwa Ujerumani" ambacho lengo lake ni kuona zinasita juhudi za kuwapokea wakimbizi.
AfD wanashangiria ushindi mkubwa kupita kiasi
Katika jimbo la mashariki la Saxony Anhalt,AfD wamejipatia asili mia 24 ya kura-idadi kubwa kabisa kuwahi kujikusanyia chama chochote cha siasa kali za mrengo wa kulia katika uchaguzi wa jimbo humu nchini. Lakini hata katika jimbo "linalosifiwa" la Baden-Wuerttemberg ambako hali ya kiuchumi inanawiri na idadi ya wasiokuwa na kazi ni ndogo,AfD wamejipatia asili mia 15 ya kura. Na huko pia kila mkaazi mmoja kati ya wawili anahofia wimbi la wakimbizi lisije likawa sababu ya kukabiliana na shida katika soko la ajira,nyumba,kuongezeka uhalifu na kuenea dini ya kiislam.
Matokeo ya uchaguzi yanaangaliwa kuwa ni pigo kwa kansela ambae ndie mshika bendera katika sisa ya wakimbizi. Katika ngome yake ya zamani Baden Wuerttemberg,chama chake cha Christian Democratic kimepoteza kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1952 usukani . Hata katika jimbo la Rhineland Palatinate na Saxony Anhalt CDU wamepoteza kura. Kufungwa njia ya Balkan na Austria na mataifa ya kusini mashariki ya Ulaya ndio sababu pigo halikuwa kubwa sana kwa CDU. Asili mia 70 ya wapiga kura wamebainisha "wameshusha pumzi" kuona wakimbizi hawaingii tena kwa wingi nchini Ujerumani.
Wajerumani walio wengi wanaridhika na kazi ya kansela Merkel
Wakati huo huo ni ni onyo kwa serikali kuu mjini Berlin isiruhusu tena mikururo mikubwa ya wakimbizi. Chama ndugu cha Christian Social Union CSU wanahisi hawajakosea katika msimamo wao dhidi ya sera za milango wazi za kansela .
Siku nne kabla ya mkutano pamoja na Uturuki mjini Brussels,kansela Merkel anajikuta akitiwa kishindo mpaka katika Umoja wa Ulaya. Hata hivyo matokeo ya uchaguzi wa jana hayatakuwa sababu kwa Angela Merkel kujiuzulu. Kwanza kwasababu hakuna ishara kwamba katika bunge la shirikisho kuna uwezekano wa kuibuka upinzani dhidi yake na pili,licha ya mzozo wa wakimbizi idadi kubwa ya wajerumani wanasema wanaridhika na kazi inayofanywa na kansela Angela Merkel kwa jumla.
Mwandishi:Gräßler,Bernd/Hamidou Oummilkheir
Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman