Zuma akanusha kutafautiana na waziri wake wa fedha
14 Septemba 2016Ukuaji huo anaousema Rais Zuma unaripotiwa kuwa ni katika robo ya pili ya mapitio ya kiuchumi, lakini hapo hapo kuna wasiwasi kuwa huenda Afrika Kusini ikashindwa kuhimili ustawi huo katika uchumi wake.
Kumekuwepo mvutano baina ya ofisi ya rais na Hazina hadi kufikia hatua ya kuanzishwa uchunguzi dhidi ya Waziri Gordhan na kikosi maalum cha uchunguzi kilichoanzishwa wakati waziri huyo alipopata madaraka kubaini endapo anahusika na makosa ya ukwepaji kodi.
Wakosoaji hata hivyo wanasema, hatua hiyo inalenga kumng'oa Gordhan kutoka kwenye wadhfa wake, ingawa Rais Zuma anakanusha. Mvutano huo unasababisha hali ya wasiwasi katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa wa viwanda barani Afrika.
Awali, Gordhan alikiuka samansi ya polisi iliyomuhusisha na uchunguzi uliokuwa ukitafuta kubaini iwapo waziri huyo wa fedha aliwatumia mashushushu wa kutoka kitengo kinachoshughulikia maswala ya kodi kuwachunguza wanasiasa akiwemo Rais Zuma juu ya ubadhirifu wa fedha za serikali.
Mzozo wa Zuma na Gordhan
Gordhan ameitetea hatua yake hiyo kwa kusema, haoni kama alifanya kosa lolote huku wanasiasa wa vyama vya upinzani wakiitaja hatua ya kubughudhiwa na polisi waziri huyo wa fedha ni sawa na kutaka kumkomoa tu.
Mfarakano umeongezeka zaidi ndani ya chama kinachotawala cha ANC tangu chama hicho kiliposhindwa vibaya kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwezi uliopita, huku wakosoaji wakiulaumu mvutano baina ya Rais Zuma na Waziri Gordhan kuwa utaathiri uwezo wa kifedha wa nchi hiyo katika soko la kimataifa.
Wakati huo huo, Rais Zuma amelalamika juu ya vitendo vya kuzomewa na wanachama wa upinzani kila mara anapotaka kulihutubia bunge.
Wabunge wa Chama cha Wapigania Ukombozi wa Kiuchumi (Economic Freedom Fighters - EFF) kinachoongozwa na Julias Malema walitoka nje ya bunge katika kitendo cha kuvuruga kimakusudi pale Zuma alipokuwa akijibu maswali ya wabunge.
Wakati yote hayo yakijiri, waziri wa fedha amewaarifu viongozi wa wafanya biashara kuwa Afrika Kusini bado ina asilimia 50 ya nafasi ya kuepuka kuteremshiwa uwezo wake wa kifedha katika soko la kimataifa.
Mwandishi: Zainab Aziz/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf